Ads

DOKIN ORGANIC FARMING YAENDELEZA KILIMO HAI, YAHAMASISHA CHAKULA SALAMA

 


DAR ES SALAAM: Kampuni ya Tanzania, Dokin Organic Farming, imeendelea kuhamasisha kilimo ekolojia (organic farming) na matumizi ya bidhaa salama na zenye virutubisho kwa jamii.

Kampuni hiyo inashiriki katika maonyesho ya viwanda yanayofanyika Viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, maarufu Saba Saba, jijini Dar es Salaam, ikionyesha bidhaa zinazotokana na kilimo hai, zikiwemo unga wa ndizi na unga wa maboga.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, uongezaji thamani wa mazao unalenga kuongeza kipato kwa wakulima na kuwapatia walaji bidhaa salama zinazozingatia afya na mazingira.

Katika maonyesho hayo, Dokin Organic Farming pia inashirikiana na wanafunzi wa Agribusiness kutoka vyuo vikuu nchini, kwa kuwapa fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu uongezaji thamani wa mazao na upatikanaji wa masoko. Ushirikiano huo umewezeshwa na TAPIA, huku kampuni ikishirikiana pia na Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM) katika kuendeleza kilimo hai nchini.

Akizungumza katika maonyesho hayo, Docas Emily Kibona, Profesa wa Chakula na Uponyaji kutoka Dokin Organic Farming, amesema lengo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kilimo hai, uongezaji thamani wa mazao na umuhimu wa chakula salama.

“Tuko hapa kutoa elimu kuhusu kilimo hai, kuhakikisha mazao yanaongezewa thamani na bidhaa salama na zenye virutubisho zinamfikia mlaji,” amesema Profesa Kibona.

Ameongeza kuwa elimu kwa wakulima na wananchi ni muhimu katika kukuza kilimo kinacholinda mazingira, kuboresha afya ya jamii na kuongeza thamani ya mazao.

Dokin Organic Farming imewahimiza wananchi na wadau wa kilimo kutembelea banda lake katika maonyesho hayo ili kupata elimu kuhusu kilimo ekolojia, uongezaji thamani wa mazao na chakula salama.

No comments