Ads

Bolt Yaongeza Kasi ya Uzingatiaji wa Sheria Sekta ya Usafiri wa Mtandao.

 Bolt Yaongeza Kasi ya Uzingatiaji wa Sheria Sekta ya Usafiri wa Mtandao, Yafadhili Leseni za LATRA kwa Madereva 5,000



Kampuni inayoongoza kwa huduma za usafiri wa kidijitali nchini, Bolt Tanzania, imeanzisha mpango mpya wa kuongeza uzingatiaji wa sheria katika sekta ya usafiri wa mtandao kwa kufadhili leseni za LATRA kwa madereva zaidi ya 600 ndani ya mwezi Agosti, huku ikilenga kufikisha zaidi ya madereva 5,000 ifikapo mwisho wa mwaka 2026.


Kwa mujibu wa kampuni hiyo, hatua hiyo inalenga kuharakisha uzingatiaji wa sheria, kuimarisha usalama wa abiria na kuongeza taaluma katika sekta ya usafiri wa mtandao nchini.

Gharama ya leseni moja ya LATRA ni kati ya Sh30,000 na Sh60,000, kutegemeana na aina ya chombo cha usafiri, mbali na gharama za mafunzo.


 Leseni hiyo humruhusu dereva kutoa huduma za usafiri wa abiria kwa mujibu wa sheria pamoja na kupata ruhusa ya kutumia maeneo mengi zaidi ya umma kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria. Kwa lengo la kufadhili zaidi ya madereva 5,000, uwekezaji wa Bolt unatarajiwa kuzidi Shilingi milioni 300, ukiakisi ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali katika kuimarisha uzingatiaji wa sheria, usalama na utulivu katika sekta ya usafiri.

Mpango huo unakuja wakati uzingatiaji wa sheria ukiendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha usalama barabarani na kujenga imani ya watumiaji wa huduma za usafiri. 


Takwimu za LATRA zinaonesha kuwa mamlaka hiyo ilitoa leseni 91,178 za magari ya kukodi katika mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurasimisha na kusimamia sekta hiyo.

Akizungumzia mpango huo, Meneja Mkuu Mwandamizi wa Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole, alisema uzingatiaji wa sheria unapaswa kuonekana kama uwekezaji wa pamoja katika usalama wa usafiri, badala ya kuwa wajibu wa kisheria pekee.



"Dereva mwenye leseni siyo tu anayekidhi matakwa ya sheria, bali ni anayethibitisha kuwa amefikia viwango vinavyohitajika kutoa huduma salama na yenye taaluma. Tanzania ina mahitaji makubwa ya usafiri, na tunahitaji madereva wengi zaidi wanaokidhi viwango hivyo. 


Kwa kufadhili leseni hizi, tunawekeza kwa madereva, tunaimarisha imani ya umma na tunachangia uendelevu wa sekta ya usafiri wa kidijitali. Dhamira yetu haiishii kwa kufadhili leseni 5,000 pekee. 


Bado kuna madereva wengi wanaoshindwa kumudu gharama za leseni, na tunaamini sekta inaweza kufikia uzingatiaji wa sheria kwa asilimia 100 ikiwa wadau wote watashirikiana."

Bolt imesema mpango huo unalenga kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyowazuia baadhi ya madereva kukamilisha mahitaji ya kisheria na hivyo kukosa sifa za kujiunga na jukwaa hilo na kunufaika na fursa za kipato zinazotolewa na kampuni hiyo.

No comments