ADO SHAIBU : ACT WAZALENDO IKO TAYARI KUSHIRIKIANA NA WADAU KUPATIKANA KWA KATIBA MPYA
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema chama hicho kiko tayari kushirikiana na wadau wengine kusimamia na kushinikiza upatikanaji wa Katiba Mpya, akiwataka vijana kutodanganywa na kauli za Serikali kuhusu suala hilo.
Ado ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoandaliwa na Ngome ya Vijana Taifa ya ACT-Wazalendo.
Amesema vijana wana wajibu wa kuendelea kudai Katiba Mpya, akidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake hawajaonyesha nia ya dhati ya kutekeleza matakwa ya umma kuhusu suala hilo.
“Tusidanganyike na maneno yao kwamba Katiba Mpya ipo kwenye ilani yao. Tusidanganyike na hotuba zao. Haya ni maneno ya kupoteza muda tu,” amesema Ado.
Amesema ACT-Wazalendo, kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kusimama imara kushinikiza CCM kukubali matakwa ya wananchi ya kuwa na Katiba Mpya.
“Kwa vile CCM na Serikali yake hawapo tayari kutuletea Katiba Mpya, sisi tunao wajibu wa kuwalazimisha kupambana nao ili wakubali matakwa ya umma ya kuleta Katiba Mpya,” amesema.
Ado pia amesema chama hicho kinaamini kuwa suala la Katiba Mpya linapaswa kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya vijana, akieleza kuwa ujumbe huo umepewa nafasi katika shughuli za vijana wa ACT-Wazalendo.
Aidha, ametangaza kuzinduliwa kwa sare maalum yenye ujumbe wa “Katiba Mpya Msingi wa Maendeleo ya Vijana,” ambayo amesema inalenga kuwasilisha ujumbe huo kwa mtazamo unaoendana na kizazi cha vijana wa sasa, hususan Gen Z.
Amesema sare hizo ni chache kwa awamu ya kwanza na zitazinduliwa rasmi na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo.
Ado amehitimisha kwa kuwataka vijana wa ACT-Wazalendo kusimama pamoja katika kudai Katiba Mpya, akisisitiza kuwa suala hilo ni muhimu kwa maendeleo na mustakabali wa vijana nchini.

Post a Comment