ISMAIL JUSSA ATETE NA NGOME YA VIJANA ACT WAZALENDO
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismaili Jussa, amewataka vijana nchini kuwa mstari wa mbele katika kudai mabadiliko ya kisiasa na katiba mpya, akisisitiza kuwa mustakabali wa taifa ni jukumu lao.
Jussa amesema vijana hawapaswi kuwa wafuasi wa viongozi bila kuhoji, bali wanapaswa kuwapa changamoto viongozi wa vyama vyao na viongozi wa serikali ili kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa wananchi.
“Kataeni kuwa chawa. Kazi ya vijana ni kuwapachallenge viongozi,” amesema Jussa.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoandaliwa na Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo jijini Dar es Salaam, Jussa amesema kizazi chake kilishiriki mapambano ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, hivyo vijana wa sasa wanapaswa kuendeleza safari hiyo kwa kudai Katiba Mpya inayokwenda na mahitaji ya wakati huu.
Amesema ACT-Wazalendo haipaswi kutafsiriwa au kupimwa kwa misimamo ya vyama vingine, akisisitiza kuwa katika mfumo wa vyama vingi, vyama vinaweza kukubaliana kuhusu malengo fulani bila kulazimika kuwa na mtazamo mmoja kuhusu namna ya kuyafikia.
Jussa ametoa mfano wa masuala ya Katiba Mpya, mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi, haki na amani, akisema masuala hayo yanaweza kuwa ajenda za pamoja, lakini njia ya kuyafikia inapaswa kujadiliwa na kukubaliwa kwa pamoja.
Aidha, amekumbusha historia ya kisiasa Zanzibar, akieleza kuwa chama chake na watangulizi wake waliwahi kuchukua misimamo mikali kuhusu uchaguzi na mfumo wa utawala, huku vyama vingine vikichagua kutounga mkono misimamo hiyo.
Kwa mujibu wa Jussa, historia hiyo inapaswa kuwa somo kwa vijana wa ACT-Wazalendo kutokubali kuitwa wasaliti kwa sababu tu wanachukua msimamo tofauti na vyama vingine.
Akizungumzia makubaliano yaliyofikiwa Zanzibar, Jussa amesema mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika si ya kuanza majadiliano mapya, bali ni ya utekelezaji wa makubaliano yaliyokwishaafikiwa.
Amesema miongoni mwa masuala yaliyomo katika makubaliano hayo ni kuandika upya Katiba ya Zanzibar pamoja na kufanya mageuzi katika mfumo wa uchaguzi, ikiwemo Tume ya Uchaguzi.
“Katika makubaliano ya Zanzibar ni pamoja na kuandika upya Katiba ya Zanzibar. Ikiwa kuna suala la Tume Huru ya Uchaguzi, katika makubaliano ya Zanzibar kunazungumzwa mageuzi ya mfumo wote wa uchaguzi,” amesema.
Jussa amesema hatua hizo zinaonesha kuwa ACT-Wazalendo tayari imeanza safari ya kudai mabadiliko kutoka Zanzibar, akiwataka vijana kutokubali kutembea kwa unyonge wala kuruhusu wengine kuwafafanulia wanachopaswa kuamini au kusimamia.
Kuhusu uwezekano wa kupata Katiba Mpya Tanzania, Jussa amesema watawala wanaonufaika na mfumo uliopo hawawezi kuwa na utayari wa kuubadilisha kwa hiari, hivyo wananchi na vyama vya siasa wanapaswa kuendelea kudai mabadiliko.
Amesema vyama vya siasa havipaswi kutegemea serikali ya CCM kutoa “roadmap” ya upatikanaji wa Katiba Mpya, bali vinapaswa kujenga mkakati wa pamoja wa kudai mabadiliko hayo.
Jussa amesisitiza kuwa hatua hiyo haiwezi kufanikiwa ikiwa kila chama kitafanya harakati zake peke yake, akitoa wito wa ushirikiano miongoni mwa vyama na wadau mbalimbali katika kudai mageuzi ya kisiasa nchini.

Post a Comment