LUHAGA MPINA AWATAKA VIJANA ACT WAZALENDO ,KUAMKA KUJENGA TAIFA LENYE NGUVU
Na Maandishi wetu, Dar es Salaam -
Naibu Waziri Mkuu wa Kivuli na Waziri wa Nishati na Madini wa Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, amewataka vijana nchini kuwa mstari wa mbele katika kupigania Katiba Mpya na kudai uwajibikaji katika uendeshaji wa Serikali.
Mpina aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoandaliwa na Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, akisisitiza kuwa taifa haliwezi kujengwa kwa nguvu bila kuwa na vijana wenye ujasiri, maono na utayari wa kushiriki katika masuala ya kitaifa.
Alisema vijana ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kujitambua, kuwa na maono na kutumia ipasavyo elimu na uwezo walionao katika kulijenga taifa.
“Huwezi kutengeneza taifa lenye nguvu halafu una vijana dhaifu, vijana ambao hawana ujasiri, hawana maono na hawana uchungu,” alisema Mpina.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili vijana, Mpina alisema ukosefu wa ajira ni miongoni mwa matatizo makubwa, akidai kuwa hata baadhi ya Watanzania wenye elimu ya juu wanakosa ajira kutokana na uchumi kutokuwa na uwezo wa kuzalisha nafasi za kutosha za ajira.
Alisema hali hiyo inahitaji mabadiliko ya sera na mifumo ya kiuchumi ili kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajiriwa.
Katika hatua nyingine, Mpina alisisitiza umuhimu wa Katiba Mpya, akisema vijana wa ACT-Wazalendo wanapaswa kuwa na jukumu la kuhakikisha mchakato wa kudai Katiba Mpya unaendelea.
Aidha, aliikosoa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kile alichodai kuwa ni ukiukwaji wa sheria na Katiba, akitaka Serikali kuwajibika na kulinda rasilimali za taifa.
“Mna kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba mnaipiga marufuku Serikali ya Awamu ya Sita kuvunja sheria za nchi, kuuza rasilimali za taifa na kuruhusu wizi, rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma,” alisema.
Mpina pia alizungumzia madai yaliyotolewa na viongozi wa kisiasa kwamba baadhi ya viongozi wa ACT-Wazalendo “wameishiwa nguvu”, akisema yeye hajawahi kuogopa mapambano ya kisiasa.
Alisema pingamizi zilizowahi kuwekwa dhidi ya ushiriki wake katika uchaguzi hazikumfanya akate tamaa, bali anaendelea kuwa tayari kushiriki katika mapambano ya kisiasa.
Akihitimisha, Mpina aliwapongeza vijana wa ACT-Wazalendo kwa maandalizi ya maadhimisho hayo na kuwataka kutumia nafasi yao kushiriki kikamilifu katika masuala ya taifa.
“Ujana ni kujitolea,” alisema.




Post a Comment