WAANDISHI WA HABARI WAHIMIZWA KUJIUNGA NA MPANGO WA SCHEME NSSF.
Mwambawahabari:
Mtunza Hazina wa Taifa wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Dk. James Kalanje amewataka waandishi wa habari nchini kujiunga na mpango wa Hifadhi Scheme wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), akieleza kuwa hiyo ndiyo njia salama ya kujenga maisha yenye uhakika baada ya kustaafu kazi.
Dkt . Kalanje ameeleza hayo jijini Dar es Salaam leo Julai 24,2026 wakati wa Mafunzo ya siku moja kuhusu mpango wa hifadhi hiyo ya Scheme, mafunzo hayo yametolewa na NSSF kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA).
Amesema waandishi wa habari ni miongoni mwa makundi yanayofanya kazi katika mazingira magumu na yenye hatari, lakini wengi wao bado hawana kinga ya hifadhi ya jamii, hali inayowafanya kuwa katika mazingira magumu wanapopatwa na changamoto za kiafya au wanapostaafu.
Amesema waandishi wa habari hufanya kazi usiku na mchana, wakati wa jua na mvua, kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati, lakini mchango wao haujaambatana na ulinzi wa kutosha wa maisha yao ya baadaye.
"Waandishi wa habari hufanya kazi usiku na mchana, kwenye jua na mvua, bila kujali hatari wanazokutana nazo ili kuhakikisha taifa linapata taarifa sahihi kwa wakati. Lakini ni jambo la kusikitisha kuona wengi wao, hasa wa sekta binafsi na wanaojiajiri, bado hawana kinga rasmi ya hifadhi ya jamii," amesema Dk. Kalanje
Amesema takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini hawajajiunga na mifuko rasmi ya hifadhi ya jamii, jambo linalowaweka katika mazingira magumu wanapougua, kupata
Amefafanua takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini hawajajiunga na mifuko rasmi ya hifadhi ya jamii, jambo linalowaweka katika mazingira magumu wanapougua, kupata ulemavu au kupoteza uwezo wa kuendelea kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Dkt. Kalanje, amesema mpango wa Hifadhi Scheme wa NSSF ni fursa muhimu inayowaruhusu wafanyakazi wa sekta binafsi na wanaojiajiri kuweka akiba kulingana na uwezo wao, huku wakijenga msingi wa maisha bora ya baadaye.
"Akiba haimtupi mtu. Ukianza kuweka akiba leo, unajenga kesho yako.
Hifadhi Scheme ni uwekezaji usio na hasara kwa sababu unakupa usalama wa kifedha baada ya kipindi cha kazi," amesema.
Ameongeza kuwa pamoja na mafao ya hifadhi ya jamii, wanachama wa mpango huo pia hupata fursa ya bima ya afya, jambo ambalo alisema ni muhimu kwa kuzingatia changamoto za gharama za matibabu zinazowakabili Watanzania wengi.
Aidha amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao, vipindi vya redio na televisheni pamoja na majukwaa ya mitandao ya kijamii kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii.
"Ninyi ni wataalamu wa habari na mawasiliano. Mkienda mikoani baada ya semina hii, tumieni kalamu zenu, vipindi vyenu na mitandao ya kijamii kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii.
Lakini kabla ya kuwaelimisha wengine, hakikisheni ninyi wenyewe mmejiandikisha kwenye Hifadhi Scheme ya NSSF," alisisitiza.
Amewataka wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari kuwahamasisha wafanyakazi wao kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha wanakuwa na maisha yenye usalama wa kifedha wanapomaliza utumishi wao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma aliipongeza NSSF kwa kuendelea kuwafikia waandishi wa habari na makundi mengine yaliyo katika sekta isiyo rasmi, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika mifumo ya hifadhi ya jamii.
Amesema uwekezaji katika hifadhi ya jamii ni msingi wa kujenga taifa lenye wananchi wenye usalama wa kijamii na kiuchumi, huku akiwataka waandishi wa habari kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kujiandikisha katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Naye Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleimani Msuya amesema chama hicho kina jumla ya wanachama 500, kati ya hao Dar es Salaam wapo 150 huku akitaja baadhi ya mikoa mengine chama hicho kinawanachama ni Dodoma, Geita, Mara, Kigoma, Mbeya, Iringa, Lindi, Mtwara na Morogoro.
"Jambo hili la NSSF lisiichie hapa Dar es Salaam, kama tulivyowahamasisha wanachama hawa kuja leo ndivyo tutkavyowahamaisha wanachama wa mikoani pia kushiriki mafunzo na kupata uelewa," amesema na kuongeza kuwa
"Kwa mujibu wa takwimu, kuna jumla ya waandishi 3500 waliosajiliwa na Bodi ya Ithibati, hata hivyo asilimia 80 hawapo katika mfuko wa hifadhi ya jamii, NSSF mkifanyakazi na sisi JOWUTA ni raisi kuweza kulifikia kundi hilo la waandishi," amesema..




Post a Comment