Ads

TAWA YASEMA VIVUTIO VYA WANYAMAPORI VIMEONGEZWA MAONESHO SABASABA

 


Simba wakiwa kwenye Banda la maonesho ya Sabasaba



Mhifadhi Mkuu wa TAWA Stephen Madenge akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo)kuhusu mazao ya vivutio vya sabasaba


Banda la TAWA katika maonesho ya 50 ya kimataifa ya biashara Dar es salaam(Sabasaba)



Mwamba wa habari
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeongeza wanyamapori pendwa, wakiwemo Twiga na Tembo, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza katika Bustani ya Wanyamapori iliyopo ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, Afisa Mhifadhi Mkuu wa TAWA, Stephen Madenge, alisema hatua hiyo inalenga kuwapa wananchi fursa ya kuwaona wanyamapori ambao hawakuwepo katika maonesho ya mwaka uliopita.

"Maonesho ya mwaka huu ni ya kipekee. Bustani yetu imesheheni wanyamapori mbalimbali, wakiwemo Twiga na Tembo ambao wameongezwa kwa mara ya kwanza katika maonesho haya," alisema.

Alisema mbali na Twiga na Tembo, bustani hiyo pia ina Simba, Chui, Duma, Pundamilia, Pofu, Nyumbu, Fisi, Mamba, spishi mbalimbali za ndege na aina tofauti za nyoka.

Madenge alisema TAWA pia imefungua duka la kuuza nyara za wanyamapori lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na wageni wanaotembelea maonesho hayo.

Aidha, alisema mamlaka hiyo imeandaa safari za kutembelea Hifadhi ya Pande iliyopo Dar es Salaam kwa gharama ya Sh35,000 kwa mtu, ambapo safari hizo zinaanzia katika viwanja vya Sabasaba.

Aliongeza kuwa TAWA, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeandaa mbio za Pande Msakuzi Marathon zitakazofanyika Agosti 1, 2026 katika Hifadhi ya Pande, huku usajili wa washiriki ukiendelea katika banda la TAWA.

Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yalifunguliwa rasmi Julai 3, 2026 na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, akiwa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026.

No comments