Tesha aichangia FFC Milioni 10, ataka Wanakwaya wajikomboe kiuchumi kupitia miradi
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Victor Tesha, amewataka wanakwaya wa Flying Family Choir (FFC) kuanzisha miradi ya maendeleo itakayokuwa chanzo cha kuongeza kipato na kuwasaidia kujikomboa kutoka katika umaskini.
Tesha amesema hayo jana, Jumapili, katika tamasha la kwaya hiyo lijulikanalo FFC Corporate Encore 2026, lililofanyika katika Ukumbi wa Cardinal Rugambwa, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, akiwemo Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Lazarus Msimbe.
FFC Kwaya inaundwa na wanakwaya kutoka madhehebu matatu ya Kikristo ambayo ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa la Anglikana na Kanisa Katoliki, wakishirikiana kupitia huduma ya uimbaji wa injili.
Akizungumza katika tamasha hilo, Tesha ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), amesema wanakwaya wengi bado wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi na hali zao za maisha si za kuridhisha, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mradi endelevu utakaoweza kuwanufaisha hata katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Amesema uwepo wa mradi mkubwa wa kwaya utasaidia kujenga ustawi wa wanakwaya na kuhakikisha huduma ya uinjilishaji inaendelea sambamba na kuimarika kwa maisha yao ya kiuchumi.
"Ningependa kuona wanakwaya wakifikiria zaidi kuhusu uwekezaji na miradi itakayowasaidia kujikomboa kiuchumi. Wengi bado hali zao si nzuri, hivyo tunahitaji kuwa na mradi ambao hata baada ya miaka 10 utakuwa umebadilisha maisha ya wanakwaya," amesema Tesha.
Aidha, ameahidi kukaa pamoja na bodi ya kwaya hiyo ili kujadili namna bora ya kupata mradi mkubwa na wenye tija ambao utalenga kuinua vipato vya wanakwaya na kuimarisha ustawi wao wa kiuchumi.
Kwa upande wake, Katibu wa kwaya hiyo, Brigita James amesema pamoja na kwaya hiyo kumiliki vifaa vyake vya muziki, bado inahitaji kuwa na chombo chake cha usafiri kitakachorahisisha shughuli za uinjilishaji na usafiri wa wanakwaya wanapopata mialiko ya kuhudumu katika maeneo mbalimbali.
Amesema upatikanaji wa chombo hicho utapunguza gharama za usafiri na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za kwaya, hususan katika huduma za uinjilishaji zinazofanyika ndani na nje ya Dar es Salaam.
Naye Mwenyekiti wa kwaya hiyo, Innocent Fundisha amesema kwaya hiyo imefanikiwa kufanya matamasha 10 tangu kuanzishwa kwake, jambo linalowapa fahari kutokana na kuendelea kudumu katika upendo, amani na mshikamano miongoni mwa wanakwaya wake.
Fundisha amesema wanakwaya wa FFC wanatoka katika madhehebu matatu ya Kikristo ambayo ni KKKT, Anglikana na Kanisa Katoliki, lakini tofauti zao za kimadhehebu hazijawahi kuwa kikwazo katika huduma yao ya uimbaji.
Amesema umoja, upendo na mshikamano walioujenga ni ishara kuwa licha ya kutofautiana madhehebu, wote wanamuabudu Mungu mmoja katika roho na kweli, huku wakitumia muziki wa injili kuhubiri amani na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa waumini.







Post a Comment