Utekelezaji wa Mkakati wa PEN-PLUS ni mwarobain katika Kukabiliana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk. Hamadi Nyembea, amesema mkutano wa tatu wa kimataifa wa PEN-PLUS unalenga kujadili na kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, hususan kisukari, selimundu (sickle cell), magonjwa ya moyo, saratani na magonjwa ya mapafu, ambayo kwa kiasi kikubwa huathiri watoto na makundi mengine ya wananchi.
Dk. Nyembea amesema mkakati wa PEN-PLUS ulianzishwa na nchi za Afrika kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika kwa lengo la kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, hususan wale wanaopata changamoto ya kupata huduma za kibingwa katika maeneo yao.
Amesema mkutano huo ulizinduliwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwaka 2024 na kufanyika tena mwaka huu, jambo linaloonesha dhamira na mafanikio ya Tanzania katika utekelezaji wa mkakati huo.
“Tanzania ilianza kutekeleza mradi huu mwaka 2022 kwa majaribio katika Wilaya za Kondoa na Karatu. Hadi sasa zaidi ya watu 500 wamenufaika na huduma hizo, huku kliniki maalumu na huduma za kibingwa zikiwa zimeanzishwa katika maeneo husika,” amesema.
Aidha, amesema moja ya malengo ya mkakati huo ni kuwajengea uwezo watumishi wa afya ambao si mabingwa ili waweze kutoa huduma za kibingwa katika ngazi za halmashauri na hospitali za wilaya, hatua itakayowarahisishia wananchi kupata huduma karibu na maeneo yao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Dk. Nyembea, utekelezaji wa PEN-PLUS umechangia kuboresha maisha ya wagonjwa wengi, ambapo baadhi yao waliokuwa wakilazwa mara kwa mara hospitalini sasa hali hiyo imepungua kutokana na upatikanaji wa huduma bora na za karibu.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kusambaza huduma hizo katika hospitali za wilaya ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na matibabu ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Dk. Nyembea amesema takribani nchi 54 zinashiriki mkutano huo wa kimataifa, jambo ambalo linatoa fursa kwa Tanzania kujifunza uzoefu wa nchi nyingine na pia kuonesha hatua iliyofikia katika utekelezaji wa mkakati huo.
Amesema kwa sasa zaidi ya nchi 20 barani Afrika zimeanza kutekeleza PEN-PLUS, ikiwemo Tanzania.
Akizungumzia hali ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini, amesema magonjwa hayo yanaongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya maisha yanayochangiwa na utandawazi.
Amebainisha kuwa takribani asilimia 30 ya vifo vinavyotokea nchini vinahusishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, saratani, pumu, magonjwa ya akili, sonona na shinikizo la damu.
Amesema kadri idadi ya watu wazee inavyoongezeka, ndivyo hatari ya magonjwa kama shinikizo la juu la damu inavyoongezeka, hususan kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60.
Dk. Nyembea ameyasema hayo katika Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ukihusisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 54 duniani.

Post a Comment