Ads

MWELEKEO MPYA ,TANZANIA NA URUSI ZAFUNGUA NJIA MPYA ZA TEKNOLOJIA NA UZALISHAJI WA VIWANDA

 



Mwamba wa habari, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Shirikisho la Urusi unapaswa kuhamishwa kutoka kwenye historia ya urafiki na kuwa matokeo halisi ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa viwanda, uhamishaji teknolojia, uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa.


Londo alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Urusi yaliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisema Tanzania na Urusi zina fursa kubwa ya kutumia uhusiano wao wa muda mrefu kujenga ushirikiano wenye manufaa kwa mataifa hayo mawili.


Amesema tukio hilo halipaswi kuonekana kama sherehe pekee, bali liwe jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya sekta binafsi za Tanzania na Urusi.


"Leo siyo tu tukio la sherehe, bali ni jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi zetu mbili. Uhusiano wetu uliopo unatakiwa sasa kutafsiriwa katika matokeo ya vitendo yanayosaidia uzalishaji, kuongeza thamani na upatikanaji wa masoko," alisema Londo.


Alisema Tanzania inatambua mchango wa Urusi katika maeneo mbalimbali ikiwemo teknolojia, viwanda, nishati, mashine na utafiti, akieleza kuwa uwezo huo unaweza kusaidia Tanzania kufikia malengo ya kuwa nchi ya viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa zake kimataifa.


"Tunatambua namna Urusi ilivyoendelea katika teknolojia, na fursa kubwa iliyopo ni kushirikiana katika uwezo huo ili Tanzania iweze kunufaika na teknolojia, mashine, mbolea na uzoefu wa viwanda," amesema.


Londo alisema Serikali inalenga kutumia ushirikiano huo kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuongeza thamani ya bidhaa, kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza uzalishaji na kuleta ajira kwa Watanzania.


Ameongeza kuwa Tanzania ina mazingira mazuri kwa wawekezaji wa Urusi kutokana na uwepo wa rasilimali nyingi, soko la ndani, pamoja na nafasi yake ya kimkakati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla.


"Tanzania siyo tu ina rasilimali nyingi, bali pia ina soko linalokua na nafasi ya kimkakati ya kufikia masoko ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Hizi ni sababu zinazowafanya wafanyabiashara na wawekezaji wa Urusi kuja kushirikiana nasi," alisema.


Aidha, alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na Urusi katika maeneo mapya ikiwemo uzalishaji wa dawa, huduma za afya, nishati, madini, kilimo, usindikaji wa mazao, uchumi wa buluu na huduma za usafirishaji.


Londo alisema Tanzania inaweza kunufaika kwa kupata teknolojia na uzoefu wa Urusi, huku Urusi ikinufaika na fursa za soko la Tanzania na uwezo wa kuzalisha bidhaa kwa ajili ya masoko mengine.


"Fursa kubwa ipo katika ushirikiano wa uzalishaji wa pamoja, kuongeza thamani viwanda na uhamishaji teknolojia.

 Ushirikiano wetu usibaki kwenye biashara ya bidhaa pekee, bali uende kwenye uzalishaji wa pamoja," amesema.

Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuhakikisha ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi unazaa matokeo yanayoonekana kwa wananchi.


Aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania na Urusi kutumia jukwaa hilo kutafuta fursa halisi za ushirikiano, kubadilishana taarifa za masoko na kuweka mikakati ya miradi ya pamoja.


"Thamani ya mikutano hii haipo kwenye kukutana pekee, bali ipo kwenye kinachotokea baada ya mikutano. Ni lazima tutambue fursa, tukubaliane maeneo ya ushirikiano na kuanza utekelezaji wa miradi yenye tija," alisema Londo.


Apamoja na hayo amesisitiza kuwa dunia inaendelea kubadilika, hivyo Tanzania inapaswa kujiandaa mapema kwa kujenga uwezo wa viwanda, teknolojia na uzalishaji ili kushindana katika uchumi wa dunia.

Londo amewataka wafanyabiashara wa Urusi kuiona Tanzania siyo tu kama eneo la kutembelea, bali kama sehemu ya uwekezaji wa muda mrefu katika biashara, utalii, viwanda na ushirikiano wa kiuchumi.

No comments