Ads

10 kwenda kushuhudia michuano ya Kombe la Dunia, wengine 10 wapatiwa TV ya nchi 85

Benki ya CRDB Plc imehitimisha kampeni yake ya Fainali Ndo Mpango na Tembo Card Visa, ambapo washindi 10 wamepata zawadi ya kulipiwa safari ya kwenda Marekani na Canada kushuhudia michuano ya Kombe la Dunia inayoanza rasmi leo, Juni 11, 2026.

Kampeni hiyo pia imepata washindi wengine 10 ambao wamezawadiwa TV kubwa ya nchi 85 kila mmoja ili waweze kupata fursa ya kufuatilia michuano hiyo wakiwa sebuleni kwao.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha kampeni hiyo, Meneja mwandamizi kitengo cha Kadi Bw.Karington Chahe amesema kuwa kampeni hiyo ilizinduliwa Februari 12, 2026 kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya card katika kufanya miamala mbalimbali ya kidijitali

"Benki ya CRDB ilizindua kampeni tarehe 12 Februari, kampeni inayoenda kwa jina la Fainali Ndo Mpango na Tembo Card Visa, kampeni ambayo inalenga kuhamasisha matumizi ya card katika kufanya miamala mbalimbali ya kidijitali," amesema Chahe.

Na kuongeza, "Kampeni hii ilikuwa ya miezi mitatu, ambayo ilikuwa inaisha mwezi wa sita, na ilikuwa na washindi 20 kwa jumla. Katika washindi hao, washindi 10 walikuwa wanapata zawadi ya Benki kuwalipia safari ya kwenda Marekani na Canada kushuhudia michuano ya Kombe la Dunia."

Amesema washindi 10 wengine walikuwa wanajishindia TV kubwa ya nchi 85, na Benki imewazawadia TV kwa maana kwamba wale ambao hawajapata fursa ya kushinda kwenda Canada na Marekani waweze kushuhudia michuano ya Kombe la Dunia wakiwa sebuleni kwao

"Nipende kuwashukuru Watanzania wote, hususan wateja wetu wa CRDB, kwa kuwa kwenye kampeni hii tumeona hamasa kubwa sana kwa wateja wetu. 

Miamala imeongezeka kwa kiwango kikubwa, hasa miamala ya card. Hiyo ina maana kwamba mapokeo ya kampeni hii yamekuwa mazuri."

Amesema kuwa leo, Juni 11, 2026, kampeni hiyo imefungwa rasmi baada ya kupatikana washindi hao 20 na kupatiwa zawadi zao, huku akisisitiza kuwa baada ya kampeni hiyo Benki inatarajia kufanya kampeni nyingine.

"Tunafunga rasmi kampeni hii, na tumefunga kampeni hii kwa kuchezesha droo na kupata washindi saba. Washindi watatu tulikuwa tunamalizia wale washindi sita wa kwenda Canada, na washindi wengine wanne waliojinyakulia TV zao kubwa za nchi 85," amesema.

Hata hivyo, amebainisha kuwa Benki hiyo ina kampeni nyingi ambazo zitaendelea kufanyika. Hivyo, ametoa rai kwa Watanzania wote kuhakikisha wanaendelea kutumia Tembo Card zao ili waendelee kupata fursa mbalimbali ambazo Benki itaendelea kuzitoa katika kampeni zijazo.




No comments