Ads

KCMC Yaomba Mchango wa Shilingi Bilioni 25 Kujenga Kituo cha Moyo

NA FRANCISCO PETER, DAR ES SALAAM

Hospitali ya Rufaa ya Kanda inayotoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi (consultant and referral specialized hospital), K.C.M.C, imewaomba Watanzania kuchangia ujenzi wa kituo cha moyo.

Gharama za ujenzi wa jengo hilo zinatarajiwa kufikia shilingi bilioni 25 za Kitanzania, ikiwa ni pamoja na gharama za vifaa tiba na vifaa vya hospitali.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Gilliard Masenga, amesema kuwa mradi huo ukikamilika utawapunguzia wakazi wa Kanda ya Kaskazini gharama za kusafiri kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili (JKCI).

“Kutakuwa na kliniki kwa wagonjwa wanaotoka nje ya nchi kuja kutibiwa hapa nchini, jambo litakalochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya Watanzania wanaokwenda nje ya nchi kutafuta matibabu,” amesema Prof. Masenga.

Ameongeza kuwa magonjwa yasiyoambukiza (Non-communicable diseases - NCDs) kwa sasa yanachangia takribani asilimia 70 ya vifo duniani, huku magonjwa ya moyo na mishipa yakiongoza kwa kusababisha vifo hivyo.

Aidha, amesema kuwa asilimia 78 ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati. Tofauti na nchi zilizoendelea, katika nchi hizi magonjwa ya moyo huanza kuwaathiri watu wakiwa katika umri mdogo, hali inayopunguza nguvu kazi na kuathiri maendeleo ya kiuchumi.

Pia ameeleza kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuanzisha kituo cha kisasa cha matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa katika hospitali ya KCMC, kitakachotoa huduma kamili za uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji kwa wagonjwa wa moyo katika Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine ndani na nje ya nchi.

Ameomba Watanzania wa rika zote na kada mbalimbali—ikiwemo vijana, wazee, wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima, viongozi na diaspora—kuchangia mradi huo kupitia akaunti zifuatazo

  • Bank of Africa: 04563580007
  • CRDB Bank: 01506858800
  • NBC Bank: 40310194610
  • NBC Bank: 017172000770
  • Mitandao ya simu:
    • Mixx by Yas: 15175376
    • Halotel (Halopesa): 23758475

Naye Dkt. Ronald Mbwasi, ambaye ni mbobezi wa magonjwa ya moyo kwa watoto, amesema kuwa viwango vikubwa vya mafuta mabaya mwilini ni miongoni mwa sababu za magonjwa yasiyoambukiza.

Ameongeza kuwa, kati ya vifo 100 vinavyotokea Afrika, vifo 13 husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza






No comments