Ads

Kawogo Awafungulia Watanzania Fursa za Ajira Scandinavia na Denmark; Serikali Yatoa Kauli

Na Francisco Peter, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Mhe. Deus Sangu, ameshiriki hafla ya kuwaaga Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, iliyofanyika leo tarehe 27/03/2026 jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, Mhe. Sangu alipokelewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ajira, Bi. Jeni Sologo, pamoja na watumishi wa wizara hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Universal Career Development Pivot Tanzania (UCDP), Patrick Kawogo, amesema taasisi hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania kupata ajira nje ya nchi, huku matarajio yakiwa kufikia thamani ya shilingi laki tatu kupitia fursa hizo.

Ameeleza kuwa UCDP imefanikiwa kuwatafutia Watanzania ajira katika nchi mbalimbali ikiwemo Ujerumani, Scandinavia na Denmark.

Hata hivyo, amesema kwa sasa wameahirisha kupeleka wafanyakazi nchini Marekani kutokana na hali ya kisiasa na migogoro inayoendelea kimataifa.

Aidha, Kawogo amebainisha kuwa taasisi hiyo imekuwa ikiunganisha vijana na fursa za ajira, hatua inayosaidia juhudi za serikali katika kupunguza ukosefu wa ajira nchini.
Amesisitiza kuwa ajira hizo hutoa nafasi kwa vijana kuchangia uchumi wa taifa, huku akibainisha kuwa sekta ya afya ina uhitaji mkubwa wa wafanyakazi katika nchi wanazoshirikiana nazo.

“Natarajia pindi tutakapoanza kupeleka wataalamu wa afya kwa wingi, idadi ya Watanzania wanaonufaika itaongezeka kwa kiasi kikubwa, na serikali pia itanufaika zaidi,” amesema.

Mbali na kuwezesha ajira za kimataifa, UCDP imejikita pia katika kutoa mafunzo ya maendeleo ya kazi, ujuzi wa kitaaluma, pamoja na uhamasishaji wa fursa za kimataifa kwa vijana. Taasisi hiyo pia inashirikiana kwa karibu na vyuo vikuu, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).



No comments