Ads

Tuzo za TEHAMA 2026 Kuchochea Ubunifu na Ushindani wa Kidijitali

Tume ya TEHAMA (ICTC) kwa kushirikiana na Chama cha Watoa Huduma za Mtandao Tanzania (TISPA) na Kampuni ya SoftVentures inayojishughulisha na ubunifu wa kiteknolojia na maendeleo ya programu, wameandaa Tuzo za TEHAMA 2026 zinazotarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu.

Tuzo hizo zimelenga kutambua jitihada zilizofanywa na wadau wa TEHAMA na kutia hamasa kwa wale waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali ambapo TEHAMA inatumika kutoa huduma za kijamii, uzalishaji mali, utafiti, ubunifu, utawala, elimu pamoja na afya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 13, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema kuwa tuzo hizo ni njia ya kipekee ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutambua mchango wa wawekezaji, wabunifu, watafiti, wajasiriamali na wadau wengine wa TEHAMA katika kuchangia maendeleo ya Taifa na kufikia uchumi wa kidijitali.

Dkt. Mwasaga amesema kuwa tuzo hizo ni moja ya majukwaa ya kuhamasisha ukuaji wa uchumi wa kidijitali, yakilenga kuchochea uvumbuzi na ushindani wenye tija pamoja na kuleta mabadiliko ya kidijitali katika nyanja mbalimbali.

“Itasaidia kuchangia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali na Dira ya Maendeleo ya 2050, ambayo imeainisha mageuzi ya kidijitali kama moja ya vichocheo vya kufikia malengo ya dira hiyo,” amesema Dkt. Mwasaga.

Amesema kuwa Tuzo za TEHAMA 2026 zimegawanyika katika makundi 14, ambapo kila kundi litakuwa na washindi watatu, jambo litakalofanya kuwa na jumla ya tuzo 42.

Miongoni mwa tuzo zitakazotolewa katika makundi hayo ni pamoja na: Uvumbuzi katika Bidhaa au Huduma za TEHAMA; Usalama wa TEHAMA – Usalama wa Mtandao na Ulinzi wa Data; Ubora na Mabadiliko ya Kidijitali; Kijana Mwenye Mafanikio katika TEHAMA; Wanawake katika TEHAMA; Matumizi Bora ya TEHAMA; TEHAMA katika Utangazaji, Vyombo vya Habari na Uandaaji wa Maudhui.

Makundi mengine ni Tuzo ya TEHAMA Endelevu; Tuzo za TISPA kwa Mtoa Huduma Bora za Mawasiliano; Tuzo za TEHAMA katika Utafiti, Uvumbuzi na Machapisho; TEHAMA kwa Watanzania waishio Nje ya Nchi (Diaspora); Tuzo za TEHAMA kwa Maendeleo; pamoja na Tuzo Maalum ya Utambuzi kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Amefafanua kuwa maandalizi ya Tuzo za TEHAMA 2026 yanaendelea vizuri, huku akieleza kuwa utaratibu wa tuzo kuanzia maandalizi, uwasilishaji wa maombi, uchambuzi wa maombi hadi kutangaza washindi unafanywa na kamati maalum ya wataalamu kwa kufuata mwongozo uliowekwa.

“Utaratibu wote unakuwa chini ya uangalizi na ukaguzi wa Kampuni ya Deloitte, ambayo imeteuliwa kama mthibitishaji huru ili kuhakikisha mchakato wa tathmini unakuwa wazi, wa kuaminika na unaozingatia vigezo vilivyowekwa,” amesema Dkt. Mwasaga.

Ametoa wito kwa wavumbuzi, wataalamu wa TEHAMA, makampuni changa (startups), watafiti, viongozi wanawake katika teknolojia, wajasiriamali, watoa huduma, wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali kushiriki katika Tuzo za TEHAMA 2026.

Dirisha la maombi kwa washiriki wa tuzo limefunguliwa kwa wadau wote hadi Machi 15, 2026. Kwa maelezo zaidi kuhusu utaratibu wa maombi, uchambuzi, fursa za udhamini na ushiriki katika hafla hiyo, wadau wanaweza kutembelea tovuti ya tuzo: www.tehama.awards.tz

No comments