Ads

KAMPUNI CHANGA 400 ZA TEHEMA ZASAJILIWA NA ICTC

Kampuni Changa 400 za TEHAMA Zasajiliwa Tume ya TEHAMA (ICT Commission – ICTC) imefanikiwa kusajili zaidi ya kampuni changa 400 za TEHAMA hadi kufikia Desemba 2025, zikiwa katika hatua mbalimbali za ukuaji, ubunifu na utoaji wa huduma. Kati ya hizo, kampuni 161 zimekidhi vigezo vya kujiunga na programu maalum za uendelezaji na uwezeshaji, zikiwemo msaada wa kitaalamu na rasilimali.



Akizungumza na waandishi wa habari Februari 12, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa ICTC, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema usajili huo ni bure na unalenga kutambua bunifu na mahitaji ya kampuni changa ili kurahisisha upatikanaji wa mitaji na huduma za kitaalamu kutoka ndani na nje ya Serikali.

Amesema mpango huo utaongeza fursa kwa kampuni hizo kuingia sokoni, kukuza mitaji yao na kushindana kwa ufanisi zaidi. 

Pia utawezesha Tume kubaini changamoto zinazowakabili na kushirikiana na wadau kujenga miundombinu wezeshi, kutoa mafunzo ya biashara na ujasiriamali kwa kampuni za hatua ya awali (early stage), pamoja na kuwezesha mitaji kwa kampuni za hatua ya ukuaji (growth stage).

Kwa mujibu wa Dkt. Mwasaga, utambuzi huo utaongeza ufanisi katika kuwasaidia kampuni kufikia vigezo vya kupata nafuu za uwekezaji, kushiriki kwenye zabuni za umma na kupata nafuu za leseni za udhibiti chini ya mamlaka mbalimbali za Serikali.

Aidha, mpango huo utasaidia kujenga imani kwa wadau wa ndani na nje ya nchi, na kufungua fursa za majaribio ya bidhaa na huduma (pilot projects), uwekezaji na makubaliano ya kibiashara.

ICTC pia itaimarisha programu za kuzitangaza kampuni changa katika mikutano ya kitaifa na kimataifa pamoja na kupitia makubaliano ya kidiplomasia ya uwili na uwingi kati ya Tanzania na nchi nyingine.

Dkt. Mwasaga ameeleza kuwa utaratibu huo umejengwa kwa kuzingatia uzoefu wa nchi zilizofanikiwa katika uwezeshaji wa kampuni changa, ikiwemo Estonia, India, Algeria na Tunisia.

Ametoa wito kwa kampuni zote changa za TEHAMA kujisajili ili zipate utambuzi maalum na kuingizwa kwenye programu za uwezeshaji.

Usajili ni bure, na ICTC itakuwa ikitoa orodha ya kampuni zilizotambuliwa kila baada ya miezi mitatu. Orodha ya kwanza ya kampuni zilizosajiliwa hadi Desemba 2025 inatarajiwa kutolewa Februari 2026 baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa mwisho.

No comments