MAONESHO YA UBUNIFU MUHAS YALETA AHUENI SEKTA YA AFYA
Mgunduzi wa Kifaa Cha SIKU SMART, Mwanafunzi wa udaktari mwaka wa tano Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Cauthary R. Abdallah, akizungumza leo Februari 24, 2026 jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa teknolojia ya SIKU SMART ambayo imelenga kuwasaidia wanawake kufuatilia mzunguko wa hedhi kwa usahihi wakati wa Maonesho ya Pili ya Ubunifu ya MUHAS (Innovation Week 2026) yanayoendelea kufanyika chuoni hapo.
...........
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wamefanikiwa kubuni teknolojia za kisasa zitakazoboreshа sekta ya afya, zikiwemo Pawakit v1.1 na SIKU SMART.
Akizungumza Februari 24, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Maonesho ya Pili ya Ubunifu ya MUHAS (Innovation Week 2026), Mwanafunzi wa Shahada ya Uhandisi Tiba, Bw. Revocatus M. Lazaro, amesema kuwa Pawakit v1.1 ni kifaa kinacholinda na kufuatilia utendaji wa vifaa tiba hospitalini.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo ina uwezo wa kuhifadhi umeme kwa saa sita hadi nane endapo kutatokea hitilafu ya umeme, hivyo kuruhusu vifaa tiba kuendelea kufanya kazi bila kuathiri huduma kwa wagonjwa.
Aidha, kifaa kinatumia akili unde (AI) na kuchambua mwenendo wa vifaa na kutoa tahadhari mapema pindi changamoto zinapojitokeza.
Bw. Lazaro amebainisha kuwa ubunifu huo umetokana na changamoto ya kukatika kwa umeme katika hospitali, hasa maeneo ya vijijini, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa wagonjwa wanaotegemea vifaa tiba. Pia kina uwezo wa kudhibiti mabadiliko ya umeme kama upungufu au ongezeko, bila kuathiri utoaji wa huduma.
Ametoa mfano wa tukio lililowahi kutokea mkoani Morogoro ambapo mashine za maabara ziliungua kutokana na kutokuwapo kwa mfumo sahihi wa ulinzi wa umeme.
Kwa sasa, timu ya ubunifu ipo katika hatua za mwisho za usajili wa kifaa, huku wakitoa wito kwa wadau kufanya uwekezaji ili kuboresha utendaji wa kifaa hicho kwani kina umuhimu mkubwa katika sekta ya afya.
Naye, Mgunduzi wa SIKU SMART, Mwanafunzi wa udaktari mwaka wa tano MUHAS, Cauthary R. Abdallah, amesema kifaa hicho kinalenga kuwasaidia wanawake kufuatilia mzunguko wa hedhi kwa usahihi.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo itawasaidia wanaotamani kupata ujauzito pamoja na wanaotaka kuepuka mimba zisizotarajiwa.
Ameongeza kuwa ubunifu huo ni muhimu kwa wanafunzi wa kike na wanawake wanaoishi vijijini, ambako upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi bado ni changamoto.
Amesema kuwa kupitia programu za elimu shuleni, waligundua wengi hawana uelewa wa kutosha wa namna ya kufuatilia mzunguko wao, jambo lililochochea kuanzishwa utafiti wa kupata kifaa cha SIKU SMART.
Kwa sasa, kifaa hicho kipo katika hatua za mwisho za usajili, huku wadau wakihimizwa kufanya uwekezaji zaidi ili kuongeza uzalishaji na kuwafikia wanawake wengi nchini.


Post a Comment