Ads

TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO WA KIMATAIFA KUHUSU MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA AI NA MABADILIKO YA YA TABIANCHI






Na mwandishi wetu

DAR ES SALAAM 

TANZANIA  imeandaa kwa mara ya kwanza Mkutano wa Kimataifa unaojadili matumizi ya teknolojia ya Akili mnemba (AI) katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza  Leo OKtoba 8,2025 Jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo amesema teknolojia ya akili mnemba inatoa fursa ya kutabiri athari za mabadiliko ya tabianchi, kusaidia juhudi za usafi wa mazingira na kuhifadhi bioanuai.


Aidha ,amesema kwamba mkutano huo umeratibiwa na Kamati ya Wataalamu ya Teknolojia ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ambapo Tanzania ni Mwanachama wa UNFCCC na Ofisi ya Makamu wa Rais ni kiungo wa mkataba huo.


“Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa ni upatikanaji wa fedha kwa miradi ya akili mnemba inayolenga mabadiliko ya tabianchi, mafunzo na ujenzi wa uwezo kwa wataalamu wa nchi zinazoendelea na maendeleo ya miundombinu ya teknolojia na uchambuzi wa data kwa kutumia AI.


Hata hivyo , amesema mkutano huo ni fursa muhimu kwa vijana, wataalamu na taasisi za Tanzania kujifunza, kushirikiana na kunufaika na teknolojia ya AI katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.


“Mkutano huo unawakutanisha zaidi ya washiriki 200 kutoka nchi mbalimbali duniani, ukiwa na lengo la kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kulinda mazingira, hasa kwa nchi zinazoendelea.”


Kwa upande wake, Mshauri wa Rais wa katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Afrika cha Majadiliano (AGN), Dk. Richard Muyungi, amesema mkutano huu utasaidia kuchochea matumizi ya AI katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.


Amesema uamuzi wa kuitangaza Tanzania kama mwenyeji wa mkutano huo umetokana na juhudi kubwa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhimiza maendeleo endelevu na utunzaji wa mazingira, matumizi ya nishati safi kupitia teknolojia.

No comments