Ads

PROF.KABUDI AMEWATAKA WAANDISHI KUJIEPUSHA NA RUSHWA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

 





Na mwandishi wetu,


DAR ES SALAAM 


WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof.Palamagamba Kabudi amewataka waandishi wa habari kujiepusha na rushwa yaani bahasha  ya kahawia kwani ni doa,wananchi wanataka habari zenye uzito wa hoja na siyo uzito wa posho.


Akizungumza Jijini Dar es Salaam Agosti 21,2025 ,katika  mkutano wa mwisho mafunzo kwa waandishi wa habari na watangazaji wa Kanda ya Mashariki ,Profesa Kabudi  amesema kwamba rushwa hupoteza uaminifu wa Vyombo vya habari na kudhoofisha Demokrasia pamoja na kukuza ufisadi kwa kusababisha waandishi waadilifu.


Pia ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutumia vyombo vya habari kwa kutoa taarifa sahihi na kuepuka lugha za uchochezi ila kudumisha amani,utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025.


"Nitumie nafasi hii kutoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa nchini kutumia vizuri vyombo vya habari kufikisha sera na mipango ya kisiasa kwa wananchi,wanasiasa wanapaswa kutumia vyombo vya habari kwa uangalifu ili kujenga taswira mpya,pamoja na kutoa ufafanuzi na kujibu taarifa zisizo sahihi zinazoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa Taifa,"amesema Prof.Kabudi


Aidha,ameviomba vyombo vya habari kuepuka kutumia maslahi binafsi bali kufanya kazi kwa weledi na kizingatia maadili ya uandishi wa habari na kuepuka upendeleo,uzushi na lugha za uchochezi.


Hata hivyo,alibainisha mambo matano ya msingi na muhimu ambayo sekta ya habari inapaswa kutekeleza kuelekea Uchaguzi


1. Kuwajulisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao.


2. Kutoa elimu juu ya sera za wagombea.


3. Kuibua na kufuatilia ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.


4. Kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum, ikiwemo vijana na wanawake.


5. Kupambana na taarifa potofu na kuepuka kuzisambaza.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Wakili Patrick Kipangula, amesema ni kosa la jinai kwa waandishi wa habari kufanya kazi hiyo bila kuwa na Ithibati.


Amesema hayo wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa wadau wa Sekta ya Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki, kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.


"Ukisoma kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari inaeleza kuwa mtu yoyote anayetaka kufanya kazi za uandishi wa habari ni lazima awe amepewa ithibati na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, kwa hiyo hakuna mtu yoyote anaruhusiwa kufanya kazi yoyote ya kihabari isipokuwa tu awe amepewa ithibati na bodi, kwa hiyo waandishi ambao wanataka kufanya kazi ya kuripoti taarifa za uchaguzi wahakikishe wamepewa ithibati" amesema Kipangula.


Naye Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini ,DCP David Misime amesema kwamba ukiona watu wanashambulia mifumo ya ulinzi,ujue ndio tabia za  uhalifu,wahalifu wanajua ukififisha Polisi,basi watavuruga amani ya nchi ila watambue ya kwamba Jeshi hilo liko imara.

No comments