Ads

JKCI yaihamasisha jamii kupata chanjo ya homa ya ini



Na: Shose Romwald – Dar es Salaam

10/07/2025 Jamii imehamasishwa kujitokeza kufanya kipimo na kupata chanjo ya

ugonjwa wa homa ya ini ambao umekuwa tatizo kubwa katika jamii kwani virusi

vya homa hiyo vipo na vinaambukiza kwa kasi.

Rai hiyo imetolewa leo na Daktari wa usalama mahala pa kazi kutoka Taasisi ya

Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elias Birago wakati wa

maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA).

Dkt. Birago alisema virusi vya homa hiyo vinaambukiza kwa njia ya majimaji

yanayotoka katika mwili wa binadamu mwenye maambukizi ikiwemo damu,

jasho, maji ya uzazi “Amniotic fluid”, kujamiiana pamoja na matumizi ya vifaa

vyenye ncha kali vilivyotumika kwa mgonjwa wa homa ya ini.

“Lengo letu kubwa kutoa huduma hii katika maonesho ya Sabasaba ni kuikinga

jamii isipate maambukizi ya homa ya ini, wale tutakaowapima na kuwakuta na

shida tutawaelekeza namna nzuri ya kupata matibabu na kwa wale ambao wako

salama watapata chanjo kupitia maonesho haya”, alisema Dkt. Birago

Dkt. Birago alisema dalili za awali za ugonjwa huo zinaweza zisionekane lakini

ugonjwa unavyoendelea mtu anaweza kupata manjano, mwili kuchoka, ngozi

kuwasha, kupata homa, kupungua uzito hivyo kupeleka ini kushindwa kufanya

kazi.

“Tumeweza kutoa elimu na umuhimu wa kujikinga na ugonjwa wa homa ya ini

kwa jamii kupitia maonesho haya kuiwezesha jamii kujua tatizo hilo kuwa lipo na

halina dawa lakini lina kinga iwapo mtu atafanya kipimo na kupata chanjo yake”,

alisema Dkt. Birago

Dkt. Birago alisema JKCI kupitia kitengo cha Usalama mahala pa kazi kilichopo

Hospitali ya Dar Group wamekuwa wakitembelea taasisi na mashirika mbalimbali

kwaajili ya kutoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya ini.


Kwa upande wake Afisa Uuguzi wa Taasisi hiyo Florah Kasema alisema wananchi

waliotembelea banda la JKCI wamehamasika kupata chanjo hiyo ambayo wengi

wao hawakuwa wakifahamu madhara yake.

Florah alisema ugonjwa wa homa ya ini unaongezeka kwa kasi na kuathiri jamii

hivyo wataalamu wa JKCI hawataishia kutoa huduma hiyo katika maonesho ya

Sabasaba bali wataendelea kutoa elimu na chanjo hiyo katika vituo vyao vya afya.

“Ni muhimu wale wote walioanza kupata chanjo ya homa ya ini kuhakikisha

wanamaliza chanjo hiyo kwa kupata chanjo zote tatu kwa kipindi cha miezi sita

kama ambavyo wameshauriwa na wataalamu wa afya”, alisema Florah

No comments