Ads

BUNIFU ZA VETA ZINAVYO BADILISHA MAISHA

 






Mkurugenzi  Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Anthony Kasore ,  ametembelea banda la VETA katika Maonesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara Sabasaba ambapo amejionea ubunifu mbalimbali uliofanywa na walimu pamoja na wanafunzi wa taasisi hiyo, ukiwa na lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika shughuli za kila siku za kiuchumi.


Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo Julai 7,2025, Mkurugenzi huyo amesema kuwa mwaka huu VETA imekuja na bidhaa na mashine mbalimbali zinazolenga sekta ya kilimo, ufugaji, viwanda vidogo na huduma nyingine zinazowagusa wananchi moja kwa moja.



Moja ya bidhaa zilizovutia wengi ni incubator ya kutotolesha mayai inayotumia nishati ya umeme au sola, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi hususan vijijini kuongeza uzalishaji wa vifaranga na kukuza kipato.


Aidha, VETA imekuja na majiko ya kisasa yanayotumia nishati safi, sambamba na bidhaa nyingine kama sabuni, mafuta ya kujipaka, na bidhaa za viwandani zinazoonyesha uwezo wa vijana waliopitia mafunzo ya ufundi.



Mkurugenzi Kasore alisisitiza kuwa dhima ya VETA haipo tu kwenye kufundisha ujuzi, bali pia kumwezesha kijana kubuni, kuzalisha, na kuuza bidhaa, na hivyo kujipatia kipato au kuwa tayari kuajiriwa.


“Mafunzo ya ufundi siyo tu kumfundisha mtu namna ya kutengeneza kitu, bali pia kuhakikisha anaweza kuingia kwenye soko la ajira au kujiajiri mwenyewe kwa mafanikio. Kwa walioajiriwa, tunawawezesha wawe wabunifu na watekelezaji bora wa majukumu yao,” alisema.



Katika kuunga mkono maboresho ya sera ya elimu ya 2023, VETA imetenga eneo maalum kwa ajili ya watoto, likiwa na lengo la kuanzisha fikra bunifu mapema na kuwajengea watoto misingi ya ujuzi kuanzia shule za msingi hadi sekondari.


“Tunawafundisha watoto mambo ya msingi kama urembo, ususi na kazi za mikono,hii ni njia ya kuendeleza sera ya elimu ya amali,tunataka watoto waelewe mapema kuwa elimu ya vitendo ni fursa halisi ya maisha,” alisema Mkurugenzi.



Baadhi ya wahitimu wa elimu ya juu ambao walijiunga na VETA baada ya chuo, sasa wameweza kuanzisha kampuni zao kutokana na maarifa waliyojifunza ambapo VETA imekuwa kichocheo cha mabadiliko kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara na kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa tija.

No comments