Ads

Naibu Waziri Nyongo Aifunda AZAKI, Akisisitiza Ushirikiano Katika Dira 2050

 


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo (Mb.), ameweka wazi umuhimu wa majadiliano ya pamoja na ujenzi wa uelewa wa pamoja badala ya ukosoaji, ili kufanikisha upatikanaji wa Dira 2050, ambayo itatokana na maoni ya wananchi na wadau mbalimbali. 

Kauli hiyo alitoa jijini Dar es Salaam leo, alipofungua Mkutano wa Asasi za Kiraia zinazoshirikiana katika mapitio ya Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Mhe. Nyongo alisisitiza kuwa kama Serikali, wako tayari kusikiliza maoni ya wadau na wananchi ili kuhakikisha kuwa Dira 2050 inakuwa halisi na inayoendana na mahitaji ya jamii. 

Alisema kuwa wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii, aliweza kushirikiana mara kwa mara na asasi za kiraia, na alikumbusha kwamba maoni yao ya kuboresha siyo ukosoaji, bali ni mchango muhimu katika mchakato wa maendeleo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiraia ya Foundation For Civil Society, Justice Novati, aliwahimiza washiriki kuzingatia kukuza uchumi na kujenga uchumi shindani kuelekea miaka 25 ijayo, huku akisisitiza umuhimu wa ushindani kwa ngazi ya mikoa ili kufanikisha ustawi jumuishi na endelevu.

 Alishukuru serikali kwa kuhusisha asasi za kiraia katika mchakato wa uandishi wa Dira 2050, na alieleza kuwa mfano wa Kenya ambapo mikoa inashindana kwa vigezo vya kutengeneza ajira ni mzuri.

Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (UNA-Tanzania), Bw. Lucas Kifyasi, aliongeza kuwa utekelezaji wa Dira 2050 utakuwa muhimu katika muktadha wa mapinduzi ya viwanda, na kwamba suala la elimu litakuwa kipaumbele ili kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanafanikiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

No comments