Ads

WANANCHI WA DSM WATAKIWA KUWA MAKINI WANAPOUZIWA ARDHI ILI KUEPUKA MATAPELI

 Na Mwandishi wetu 

Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam na Pwani wamewashauri kuwa makini pindi wanapouzina ardhi na kuhakikisha fedha za malipo zinawekwa katika akaunti ili kuepuka utapeli.

Wito huo umetolewa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Shukrani Kyando wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 48 ya kimataifa ya Biashara sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya mwalimu Julias Nyerere Jijini Dar es salaam.

“Haiwezekani kuuza ardhi ya Sh. milioni 200 kwa milioni 50, lazima ujiulize ni kwanini auze kwa bei hiyo? usinunue ardhi kwa kuwa inauzwa kwa bei ya chini unatakiwa kujiridhisha kwanza na fedha zote ambazo unanunua ardhi zipitie kwenye akaunti ya wauzaji ili ziweze kutengeneza ushahidi wa hayo mauziano"amesema

"Kwa Mkoa wa Pwani tumebaini kwamba mauzo mengi wananchi wanapeana fedha mkononi, kwa hiyo wananchi wanatapeliwa na inakuwa ngumu kuthibitisha kwa sababu watu wengi wanakimbia na muda mwingine wanawageuka kwamba haukunipa fedha,” amesema na kuongezwa:

Amesema fedha zikipota katika akaunti zinakuwa katika usalama na kuwepo Kwa ushahidi ambapo vyombo vya kisheria vinaweza vikachukua hatua kwasababu ushahidi unakuwepo na unakuwa wa wazi.

Aidha alitoa wito kwa wananchi ambao wanamiliki Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na sehemu yoyote ile nchini wajitahidi sana kulipia gharama za upimaji kupitia makampuni ya urasimishaji au taasisi binafsi au ofisi za wakurugenzi, ili wapimiwe ardhi zao.

"Tunawashauri wananchi ambao wanamiliki Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na sehemu yoyote ile nchini wajitahidi sana kulipia gharama za upimaji kupitia makampuni ya urasimishaji au taasisi binafsi au ofisi za wakurugenzi, ili wapimiwe ardhi zao na baada ya hapo wapewe hatimiliki zao.

Amesema ni muhimu kupata hatimiliki kwaajili ya ulinzi wa ardhi zao ili waweze kuepuka migogoro inayosababishwa na ardhi.

"Usipo na ulinzi wa kisheria kwenye ardhi yako unaweza ukajikuta umeipoteza…kwahiyo tunawashauri wananchi wafuate hizo taratibu,” amesema.

No comments