Ads

KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID YAREJESHA KICHEKO KWA WANANCHI

Kupitia kampeni ya kitaifa ya Msaada wa kisheri a ya Mama Samia Legal Aid jumla ya wananchi 490,000 kutoka katika mikoa saba, wamepata suluhisho la migogoro mbalimbali kupitia Kampeni hiyo.

Kampeni hiyo iliyoanza kutekelezwa Aprili mwaka jana kwa kuanzia mkoani wa Dodoma na mpaka sasa tayari mikoa saba imefikiwa.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Mama Samia Legal Aid Campain katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaama(DITF) yanayoendelea barabara ya Kilwa wilayani Temeke.

Amesema baadhi ya migogoro ambayo imetatuliwa kupitia kampeni hiyo ni ile inayohusu ushauri wa msaada wa kisheria, kuelimishwa kwa suala lolote la kisheria pale wanapohitaji kuwasilisha mahakamani, kuwaunganisha na Mawakili, kuandaliwa nyaraka na huduma nyinginezo zinazohitaji kutatuliwa kisheria.

“Kwa hiyo Wizara iliona umuhimu wa kuleta kampeni hii ya kitaifa ya msaada wa kisheria ambayo imepewa jina mama Samia legal Aid Campain katika maonesho haya ya sabasaba kutokana na umuhimu wake katika kutatua migogoro ya wananchi na kampeni hii inatolewa bure,”alisema Eater.

“Kwa hiyo tuko hapa kuungana na wadau wengine katika kuhakikisha mwananchi hakosi huduma yoyote ya kisheria akiwa katika viwanja hivi vya sabasaba, kwa hiyo kama kuna mtu ana jambo lake linamtatiza na anataka litatuliwe kisheria atumie fursa hii ya maonesho,tuko mpaka mwisho kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi zaidi.


Ester ambaye pia ni Msajili wa Mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria, amesema kesi ambazo wakili anaweza kumsaidia mwananchi baada ya kufika katika kampeni hiyo ya kitaifa ni pamoja na hati za kufungua mashauri mahakamani iwe ni kufungua kuomba usimamizi wa mirathi, masuala ya madai,matunzo ya watoto, kuasili watoto na masuala mengine ya kisheria ambayo nyaraka zake zinapelekwa mahakamani.

Amesema pia ipo mikataba ambayo mtu anaweza kusaidiwa kuandika pamoja na huduma nyingine ambazo mwananchi wa kawaida hawezi kwenda kuzipata kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumlipa wakili.

Ester alisema tangu yalipoanza maonesho ya sabasaba Juni 28 mwaka huu, mwitikio wa wananachi wanaojitokeza kuomba kutatuliwa migogoro yao inayohitaji msaada wa sheria ni mkubwa.

“Wananchi waliojitokeza ni wengi tangu tumefika hapa Juni 28 na hii inatuonyesha kwamba huduma zetu zimefika mbali sana na wananchi wamepata taarifa kwa hiyo kadiri muda unavyoenda na idadi ya wananchi wanaokuja hapa inaongezeka,”alisema Ester.

Alisema wananchi wanapopata elimu ya kisheria na ushauri, wanakuwa na uwezo wa kuelewa taratibu za kisheria na haki zao, hivyo kupunguza malalamiko na migogoro isiyokuwa na ulazima.

“Kampeni hii inalenga kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi kwa njia rahisi na ya karibu. Kupitia kliniki za ushauri na elimu ya sheria, wananchi watapata fursa ya kushauriwa na wataalamu wa sheria bila malipo,” amesema 

Aidha amesema kampeni hiyo inalenga pia kujenga jamii yenye ufahamu zaidi na yenye uwezo wa kudai na kulinda haki zao za ardhi kwa mujibu wa sheria Kukuza usawa na haki katika jamii, 

kuheshimu matakwa ya marehemu, kuzuia migogoro ya mirathi, na kusimamia mali kwa njia inayofuata sheria na haki za kila mmoja.

“Wananchi wanahitaji msaada wa kisheria ili kupata haki zao kwa hiyo hii kampeni inatoa msaada wa kisheria kupitia vituo vya msaada, mawakili, na elimu ya kisheria, ikilenga migogoro ya ardhi, urithi, na haki za binadamu na inaongeza uelewa wa sheria na upatikanaji wa haki nchini Tanzania,” amesema

Mama Samia Legal Aid Campain pia imefikia mkoa wa Dodoma mikoa mingine iliyofikiwa ni, Manyara, Singida, Simiyu, Shinyanga na Njombe na Ruvuma.

Kampeni hiyo inachangia utawala bora ambao unajumuisha uwazi, uwajibikaji, na ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi na utekelezaji wa sheria na sera za umma.

No comments