Ads

PURA :LENGO NI KUFIKIA ASILIMIA 80 YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA WANANCHI IFIKAPO 2034.

 


Mwamba wa habari.

Mamlaka  ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imetumia  Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kuwaeleza  wananchi Miradi wanayosimamia na tafiti walizofanya kwenye mafuta na gesi asilia hapa nchini.

Akizungumza leo, Julai 12, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, alipotembelea banda la PURA katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa, alisema kuwa kutokana na ugunduzi wa gesi unaoendelea nchini, wananchi wanapaswa kutumia nishati safi ya kupikia.

Ameweka malengo ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi yafikie asilimia 80.

“Tunafanya tafiti mbalimbali ili kuwezesha jambo hili liwezekane kwa kuzalisha kiasi cha gesi ambacho kitaweza kuhudumia majumbani, katika magari, na kwenye maeneo mengine,” alisema Mhandisi Sangweni.

Alisisitiza umuhimu wa kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua mazingira kama mkaa na kuni, na badala yake kutumia nishati safi ambayo haina madhara makubwa kwa mazingira. “Tumeweka malengo ya kutumia nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034,” aliongeza.

Mpaka Sasa maeneo ambayo tayari yamegunduliwa kuwa na gesi ni pamoja na Mnazi Bay na Songosongo iliyopo Mtwara. Mhandisi Sangweni alieleza kuwa maeneo yenye viashiria vya mafuta yanajumuisha zaidi ya asilimia 50 ya eneo la Tanzania, ambapo tafiti zimefanyika katika eneo la zaidi ya kilomita za mraba 160,200, hasa katika maeneo ya Pwani.

Amefafanua kuwa maeneo hayo ni Tanga, Kusini, na Mtwara, ambapo tafiti zimefanyika hadi baharini zaidi ya kilomita 400.

Eneo hili tayari limepata kibali kutoka Umoja wa Mataifa (UN) na limeshagawanywa katika vitalu kwa ajili ya uwekezaji.

PURA inaendelea na ugunduzi katika maeneo ambayo yana viashiria vya gesi, na sasa wanatangaza maeneo mbalimbali ili kuvutia wawekezaji kushirikiana na taasisi pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) katika kutafuta na kuendeleza nishati hiyo.

Pamoja na hayo  ameeleza kuwa  PURA inaendelea na ugunduzi katika maeneo ambayo yana viashiria vya gesi ambapo imebainika kuwa ni asilimia 50 ya eneo la Tanzania.

“Kwa sasa tunatangaza maeneo mbalimbali ambayo yanavutia wawekezaji kwa ajili ya kushirikiana na taasisi pamoja na TPDC katika kutafuta na kuendeleza kinachopatika"Alisema.

No comments