Ads

CHUO KIKUU DODOMA WAJA NA UBUNIFU MAONESHO YA SABASABA

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.

CHUO  Kikuu cha Dodoma, kimesema katika  Maonesho  ya 48 ya kimataifa ya Biashara sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya mwalimu Julias Nyerere Jijini Dar es salaam wamekuja na picha walizobuni wanafunzi ikiwemo picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Idala ya Sanaa na Taaluma za habari katika chuo hicho Dkt Deograsia Ndunguru wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho hayo amesema wanafunzi wamekuwa wakifundushwa mbinu mbalimbali za uchoraji na ufanyaji sanaa.

“Tumekuja na picha walizobuni wanafunzi na mapambo ambayo ni bunifu za wanafunzi, tunawafundisha uchanganyaji wa rangi, matumizi ya rangi zenyewe, kutumia fursa zinazowazunguka ili kujipatia kipato. Mfano kuna chupa za vinywaji mbalimbali ambazo tukishakunywa tunatupa, hizo takataka ni fursa kwa wanafunzi wetu, wanaokota na kutengeneza bidhaa mpya inayoweza kuwapatia kipato,” amesema Dk. Ndunguru.

Naye Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Enock Tarimo  ambaye amechora picha ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inayomwelezea akiwa katika majukumu matatu ya kitaifa ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watembeleaji wa maonesho hayo ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba.

"Jukumu la kwanza la kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaiona picha ambayo ina ushungi mwekundu na vazi jeusi, analo jukumu la pili ambalo ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi tunamuona katika vazi la chama, ana ushungi mweusi na vazi la kijani. Jukumu la tatu tunamuona Dk. Samia Suluhu Hassan Amiri Jeshi Mkuu yuko katika vazi la kijeshi,” amesema Tarimo.

Mmoja wa wahitimu katika fani hiyo, Sultan Samwel, amesema kumekuwa na dhana potofu na hata baadhi ya wazazi kudhani kwamba sanaa ni uhuni hali inayosababisha kuwapo kwa mwamko mdogo.

“Watu wengi walikuwa hawajui kama ngazi ya chuo kikuu mwanafunzi anaweza kujifunza kuchora, tunawatengeneza wanafunzi wakimaliza masomo waweze kujiajiri. Ajira zipo lakini hazitoshi, wanaomaliza ni wengi na si wote wanaweza kuajiriwa na serikali kwahiyo tunamuandaa mwanafunzi anapotoka anakuwa tayari ana kitu cha kufanya,” amesema.

No comments