Ads

TMA YATOA TAARIFA YA MWELEKEO WA HALI YA HEWA KIPINDI CHA KIPUPWE

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema katika   kipindi cha msimu wa Kipupwe kinachotarajiwa kuanza mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, huku hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu Kusini-Magharibi, Kusini mwa Mkoa wa Morogoro pamoja na kanda ya kusini.

Akizungumza leo Mei 27, 2024 wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi, huku Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15oC na 20oC.

Dkt. Chang’a nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi pamoja na  kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 20 oC na  maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 15oC.

Amefafanua kuwa ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi.

Pia kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 23oC na 26oC kwa maeneo ya mwambao wa pwani na visiwani, na kati ya nyuzi joto 17oC na 23oC katika maeneo ya nchi kavu. Na maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 17oC.

Amesema kuwa Kanda ya magharibi kutakuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwakuwa kati ya nyuzi joto 15oCna 20oC, huku maeneno ya kusini mwa mkoa wa Katavi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali chini ya nyuzi joto 15oC.

Pia Kanda ya kati hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 11oCna 17oC

Dkt. Chang’a amesema kuwa katika msimu wa Kipupwe mwaka huu tunatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani hadi upepo mkali utakaovuma kutoka kusini-mashariki katika maeneo mengi na vipindi vichache vya upepo wa kusi katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

“Vipindi vya mvua vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani, nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma” amesema Dkt. Chang’a.

Hata hivyo amesema kuwa athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na magonjwa yanayohusianana hali ya baridi kama vile homa ya mapafu, magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza kwa   kwa kiasi kidogo.

“Kutakuwa na vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho na magonjwa mengine yanayohusiana na hali hiyo”amesema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a ametoa wito kwa mamlaka mbalimbali kuchukua tahadhari kiafya ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi kutokana na hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi katika kipindi.

Amesema kuwa wakulima wanashauri wakulima mboga mboga na mazao ya mizizi kama vile viazi, huku sekta za ujenzi, madini na uchukuzi zinaweza kunufaika kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa.

No comments