TANZANIA MWENYEJI WA MAADHIMISHO YA MIAKA 20 BARAZA LA AMANI NA USALAMA UMOJA WA AFRIKA
Na Francisco Peter ,
Dar es salaam.
TANAZANIA itakuwa Mwenyeji wa maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ambapo yatafanyika Mei 25/2024 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilianzishwa mwaka 2004. Baraza hili lilifanya Kikao cha kwanza cha Baraza la Amani na Usalama tarehe 25 Mei, 2004. Kwa msingi huo; mwaka huu, tarehe 25 Mei, Baraza litatimiza miaka 20 tangu lilipoanza kufanya kazi.
Maadhimisho hayo yataongozwana kaulimbiu isemayo "Miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ikiwa Chombo cha Maamuzi: Miongo miwili ya Afrika ya Amani na Usalama tunayoitaka.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Mei 22/2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba amesema Baraza la Amani na Usalama ni chombo cha juu kabisa cha maamuzi kuhusu masuala ya amani na usalama kwenye Umoja wa Afrika ambapo Mwezi machi 2024 katika mkutano mkuu wa 37 wa baraza hilo Tanazania ilichaguliwa kuwa mjumbe kwa mara ya pili na mwezi Mei mwaka huu ikachaguliwa kuwa Mwenyekiti kwa mwezi Mei.
"Miongoni mwa majukumu ya Baraza hili ni kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana nayo pale inapojitokeza. Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilianzishwa mwaka 2004 kuchukua nafasi ya Chombo cha Kuzuia na Kukabiliana na Migogoro (Central Organ for Conflict Prevention and Management) cha uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (Organization of African Unity - OAU),Kama mnavyofahamu, kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyotokea duniani, OAU ilibadilishwa kuwa Umoja wa Afrika" Amesema Makamba.
Ameongeza kuwa Ncchi 15 pekee Kati ya nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika ndio Wajumbe wanaounda Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.
"Kwa sasa nchi hizo 15 wajumbe wa Baraza hili ni: Tanzania, Uganda na Djibouti (kutoka Ukanda wa Mashariki); Cameroon, DRC na Equatorial Guinea (Kanda ya Kati); Afrika Kusini, Angola na Botswana (Kanda ya Kusini); Cote d’Ivoire, Gambia, Nigeria na Sierra Leone (Magharibi) na;Misri na Morocco (Ukanda wa Kaskazini)".
Pia amesema Tanzania inamchango mkubwa katika ukombozi wa bara la Afrika ambapo imejijengea heshima Duniani Kote kuwa mstari wa mbele katika kusuluhisha migogoro mbalimbali katika nchi mbalimbali Dunia pia imekuwa mstari wa mbele katika kuhimizs Amani.
Ameongeza kuwa Taifa la Tanzania kabla ya uhuru lilihakikisha Nchi zote za Afrika zinapata uhuru na baada ya uhuru kupatikana viongozi wa Tanazania wakiongozwa na Mwl. Nyerere walijikita kuhakikisha Bara la Afrika linaendelea kuwa na utulivu na amani ya kudumu.
"Tanzania tokea wakati wa Mwl. Nyerere ilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha Nchi za Afrika zinakuwa na usalama na amani ambapo mpaka leo viongozi wote waliofwata wamekuwa wakiendeleza jitihada hizo na Tanzania imekuwa ikitatua migogoro mbalimbali inayojitokeza katika nchi za Afrika,hivyo kwa jukumu tulilopewa hapa Tanzania ndio mahala pake".
Maadhimisho haya, yanatarajiwa kuhudhuriwa na wageni takriban 120 kutoka nchi mbalimbali. Miongoni mwa watu mashuhuri watakaoshiriki Maadhimisho hayo ni pamoja na Mhe. Jessica Alupo, Makamu Rais wa Uganda; Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika; Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Olesegun Obasanjo; Rais Mstaafu Burundi, Mhe. Domitien Ndayizeye; Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joachim Chissano na Mhe. Rais wetu Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa hapa nchini, wamealika takriban washiriki 700.
Aidha, katika kusherehekea Maadhimisho hayo, tarehe 24 Mei, 2024 kutafanyika Mjadala wa Wazi kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kupokea maoni yao kuhusu utendaji kazi wa Baraza na namna ya kuweza kuliimarisha.
Post a Comment