Ads

TMA YATOA UFAFANUZI KUPATWA KWA JUA

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema Aprili 8, 2024, kunatarajiwa kutokea kwa tukio la kupatwa kwa Jua Kikamilifu.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa tukio hilo linatarajiwa kutokea upande wa Bara la Amerika ya Kaskazini kupitia Mexico, Marekani na Kanada.

Aidha, tukio hilo linatarajiwa kuanzia maeneo ya kusini mwa Bahari ya Pasifiki ambapo Mexico itakuwa nchi ya kwanza kufikiwa na kupatwa kwa Jua Kikamilifu mnamo majira ya saa 5:07 asubuhi kwa saa za Amerika.

Njia ya kupatwa kwa Jua itaendelea kutokea Mexico na kuingia Texas, Marekani majira ya saa 7:40 mchana ikipita baadhi ya maeneo na kisha kuingia Kusini mwa Ontario, Kanada na kutoka Bara la Amerika ya Kaskazini kupitia pwani ya Bahari ya Atlantiki katika mji wa Newfoundland, Kanada, saa 11:16 jioni.

Imeeleza kuwa kwa sehemu ya jua inayofunikwa na mwezi wakati wa kilele cha kupatwa kwa jua kikamilifu itatofautiana baina ya eneo na eneo.

Maeneo yaliyo ndani ya njia ya kupatwa kwa jua kikamilifu yataona kupatwa kwa jua kwa kiwango kikubwa zaidi ikilinganishwa na maeneo yaliyo mbali zaidi na njia hii.

Kwa kuwa Tanzania inaangukia katika eneo la mbali zaidi na njia hiyo, hivyo haitashuhudia tukio hilo,kutokana na tukio hilo kutokea mbali zaidi na nchi yetu, athari za moja kwa moja katika masuala ya kijamii na kiuchumi hazitarajiwi kuonekana hapa nchini.

Mamlaka ya hali ya hewa inaendelea kufuatilia na itatoa taarifa za mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza katika hali ya hewa kulingana na tukio hili la kupatwa kwa jua.

No comments