MZUMBE WAFANYA UTAFITI KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo
Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Baraza la Utafiti wa Sayansi ya Binadamu
(HSRC) kutoka Nchi ya Afrika Kusini wanafanya utafiti kukabiliana na athari za mabadiliko
ya hali ya hewa na tabianchi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo.
Akizungumza
na mwandishi wetu Jijini Dar es Salaam, Msimamizi Mkuu wa Utafiti huo na
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam Dkt. Francis
Mwaijande, amesema kuwa lengo la utafiti ni kutafuta taarifa zitakazowasaidia
watunga sera nchini kujua kuna changamoto gani na maboresho yanayopaswa kufanyika
ili kuongeza usalama wa uzalishaji wa chakula.
“Kumekuwa
na changamoto katika mifumo ya uzalishaji wa chakula nchini ambazo zimetokana
na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini zipo tafiti nyingi zimefanyika na
kuonesha matumizi ya teknolojia yanaweza kuwasaidia wakulima kuongeza kasi
uzalishaji wa chakula” amesema Dkt. Mwaijande.
Dkt.
Mwaijande amesema kuwa utafiti huo utafanyika kwa muda wa miezi mitatu katika
mikoa sita ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Iringa pamoja na Njombe.
“Kuna
timu ya watafiti kutoka Afrika kusini na Tanzania tayari wamejengewa uwezo
jinsi ya kukusanya taarifa za utafiti ambazo zitakwenda kuwa msaada kwa watunga
sera kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa” amesema Dkt. Mwaijande.
Ameeleza
kuwa utafiti unakwenda kuangalia katika maeneo tofauti hasa usalama wa chakula upande wa
lishe, uzalishaji pamoja na upatikanaji.
Dkt.
Mwaijande amefafanua kuwa pia utafiti utaangalia kwa namna gani mabadiliko ya
hali ya hewa yanaweza kuongeza fursa au hasara katika uzalishaji wa chakula.
“Mabadiliko
ya hali ya hewa yanaweza kuleta mvua nyingi au upungufu wa mvua, ukiangalia
kilimo chetu kinategemea mvua, ikitokea kuna upungufu wa mvua uzalishaji wa
chakula unakuwa mdogo na kusababisha kupungua kwa usalama wa chakula” amesema
Dkt. Mwaijande.
Hata
hivyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu
Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt.
Ladislaus Chang’a, ametoa wito kwa mamlaka mbalimbali nchini kuchukua taadhari
kuhusu kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinazoweza
kujitokeza.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam wakati akitoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa
maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka Dkt. Chang’a amesisitiza umuhimu wa
sekta mbalimbali kuchukua taadhari ikiwemo kilimo na usalama wa chakula.
“Wakulima
wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika
kwa wakati, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani,
mmomonyoko wa upotevu wa rutuba pamoja na kuchukua mbegu na mazao sahihi kwa
ajili ya msimu wa masika” amesema Dkt. Chang’a.
Pia,
ameshauri kuimarisha miundombinu ya kilimo hususani maneo ya mabondeni pamoja
na kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza,
huku akiwakumbusha wauzaji na wasambazaji wa pembejeo za kilimo kuhakikisha zinapatikana
kwa wakati.
Kutokana
athari za mabadiliko ya hali ya hewa nchini Tanzania, utafiti unaofanywa na
Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Baraza la Utafiti wa Sayansi ya Binadamu
(HSRC) kutoka nchi ya Afrika Kusini
utasaidia kwa asilimia kubwa katika kutunga na kufanya maboresho ya wa sera ili
kupata majibu rafiki ya kuzuia athari zinazoweja kujitokeza.
Hivi
karibuni Taifa limeshuhudia athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa
baada ya kutokea mafuriko katika mikoa mbalimbali nchini na kuleta maafa pamoja
na kuharibu miundombinu ya uzalishaji wa chakula.
Licha ya changamoto ya
mabadiliko ya hali ya hewa nchini uzalishaji wa chakula umekuwa ukiongezeka
kila mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Waziri wa
Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema kuwa uzalishaji wa chakula nchini umeongezka
kutoka tani milioni 17.4 kwa mwaka 2022 hadi kufikia tani milioni 20 kwa mwaka
2023.
Post a Comment