PIC YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA SGR
Na Francisco Peter
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imeeleza kuridhishwa na mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa mkoani Mororogoro na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Deus Sangu baada ya Kamati kutembelea mradi huo na kushuhudia majaribio ya treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam hadi mkoani Mororogoro.
"Tumeona kazi kubwa imefanyika, tumeridhishwa mradi umetekelezwa katika viwango vizuri," amesema Sangu.
Amesema mradi huo umetoa fursa mbalimbali ikiwemo fursa za ajira laki moja na nusu na kwamba mradi wote wa SGR unagharimu shilingi trilioni 23 ambapo hadi sasa asilimia 40 ya fedha hizo zimeshatolewa.
Sangu ametaja faida za mradi huo utakapoanza kufanyakazi, na miongoni mwa faida hizo ni kwamba safari za abiria na mizigo zitakapoanza zitapunguza nusu ya muda ya ule ambao unatumiwa na mabasi.
Kadhalika amesema gharama za kusafirisha mizigo itapungua kwa asilimia 50.
Hivyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuendeleza mradi huo kwa kutoa fedha za kuutekeleza.
Hata hivyo amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kusimamia mradi huo ukamilike kwa viwango vizuri na kutunza miundombinu yake.
Sangu amewataka pia wananchi kutumia fursa ya mradi huo kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa amesema kuwa watahakikisha mradi huo unaanza kufanyakazi ifikapo mwishoni mwa Julai Mwaka huu.
Post a Comment