ACT WAZALENDO WATAKA DEMOKRASIA KATIKA UCHAGUZI
Na Francisco Peter, Dar es Salaam
Chama Cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuonyesha kwa vitendo usimamiaji wa demokrasia kutokana na chaguzi za marudio kuonesha kukosekana kwa nia ya dhati na ni dalili mbaya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho bara,Isihaka Mchinjita wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali ikiwemo chaguzi ndogo za udiwani katika kata 23 zilizofanyika March 20 mwaka huu ambazo zote Chama Cha Mapinduzi CCM ndio kilishinda.
Amesema ni muda muafaka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa na watumishi wake hadi katika ngazi ya Halmashauri ili uchaguzi usisimamiwe na Watumishi wa Halmashauri ambao wengi ni Makada wa Chama Tawala CCM.
Hata hivyo ameshauri kuanza kwa tume huru ya Uchaguzi kutokana na kuonekana kwa dosari kadhaa katika uchaguzi huo ikiwemo wapiga kura kuwa wengi kuliko idadi ya walioandikishwa na baadhi ya wagombea wao kudaiwa kutekwa na kupigwa.
Amesema kupitia muswada wa Sheria ya tume ya Uchaguzi ambao umepitishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inabidi tume ya Sasa ijiuzulu ili kupisha tume mpya huku akishauri tume hiyo mpya kuanza kuwa na watumishi wake kuanzia ngazi za juu mpaka ngazi za Halmashauri.
“Sisi ACT Wazalendo tunashauri utaratibu wa uzalishaji,uhifadhi na usambazaji wa karatasi za kupigia kura kuangaliwa upya Ikiwemo kushirikisha vyama vya siasa na wadau wengine kwenye kila hatua ili kuepusha sintofahamu, Hali inayopelekea wagombea wengine kulalamika kuibiwa kura”amesema Mchinjita.
Sambamba na hayo amesema chama hicho pia kimeshauri mapendekezo yaliyoainishwa na Tume ya Haki jinai yafanyiwe Kazi ili kuvifanyia maboresho vyombo vya ulinzi na usalama hasa jeshi la polisi katika kusimamia haki za wananchi kwa weledi na usawa huku kikishauri pia uamuzi Uliopitishwa na Bunge February 2 mwaka huu kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na Tume huru ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI uheshimiwe.
Post a Comment