TAKUKURU TEMEKE YAFICHUA 'MADUDU' UTOAJI VIBALI VYA UJENZI VITUO VYA MAFUTA
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke inawachuguza baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Ardhi kwa tuhuma za kughushi na kula njama ya kufanikisha upitishaji wa kibali cha ujenzi wa kituo cha mafuta cha Kampuni Petro Afrika bila kufata utaratibu wa kanuni na Sheria.
Hatua hiyo imekuja baada TAKUKURU Mkoa wa Temeke kufanya uchuguzi na kujiridhisha kisha kuwasiliana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ndugu Elihuruma Mabelya juu ya taarifa hiyo na kuchukua hatua ya kusimamisha ujenzi wa kituo cha mafuta ambao uliokuwa unaendelea katika kiwanja namba P. 18435 katika eneo la Mbagala.
Akizungumza na waandishi wa habari leo February 5, 2024 Jijini Dar es Salaam Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Eugenius Hazinamwisho, amesema kuwa wanaendelea kukamilisha uchunguzi ili wote waliohusika waweze kufikishwa Mahakamani.
"Uchunguzi wa kina kuhusu kutolewa kwa kibali hicho cha ujenzi ulibaini kwamba, wapo baadhi ya watumishi wachache wasiowaadilifu wa Wizara ya Ardhi walikula njama na kufanikisha upitishaji wa Kibali cha ujenzi huo kinyume na sheria" amesema Bw. Hazinamwisho
Bw. Hazinamwisho amesema kuwa taarifa hiyo imepatikana kupitia utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU Rafiki ambapo wadau walitoa kero y kituo cha Mafuta cha Kampuni PETRO AFRICA kinajengwa bila kufuata utaratibu na kinyume na kanuni namba 93 za Mipango Miji za 2018 zinazoelekeza umbali wa kituo kimoja hadi kingine kuwa mita 200.
Amefafanua kuwa tangu uchunguzi ulipoanza, wameendelea kupokea taarifa zinazoonyesha kwamba, vipo vibali vingine kwenye maeneo mbalimbali nchini vilivyotolewa kinyume cha sheria, huku akieleza kuwa uchunguzi huu utakuwa endelevu ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na ujenzi huo holela wa vituo vya mafuta.
"Nitumie fursa hii kutoa Rai kwa wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo vya mafuta katika Mkoa wa KITAKUKURU wa TEMEKE, kabla ya kuanza mchakato wa kuomba vibali vya ujenzi wajiridhishe na matakwa ya sheria za mipango miji Sura ya 355 na Kanuni zake za 2018" amesema Bw. Hazinamwisho.
Ameeleza kuwa wawekezaji na wafanyabiashara wanapaswa kufata utaratibu vinginevyo wanawezwa kuunganishwa kwenye mashtaka ya kula njama kutenda vitendo vya rushwa vikisomwa pamoja na makosa ya Uhujumu uchumi kwa kuwa k/f cha 8 Sheria ya Kanuni za adhabu Sura ya 16 kinaeleza wazi kwamba kutokujua sheria hakuwezi kuwa utetezi wa kutenda makosa ya jinai.
Katika hatua nyengine amesema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Temeke wamefanikiwa kufatilka utekelezaji wa miradi ya maendelo 6 yenye thamani ya Shs 2,120,255,229.73.
Amesema kuwa kati ya fedha hizo Shs 623,998,425 ni fedha za miradi ya Manispaa ya Kigamboni na sh 1,496,356.804.75 ni fedha za miradi ya Manispaa ya Temeke.
Amesema kuwa miradi husika katika Manispaa ya Temeke ni ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Kibondemaji, Ujenzi wa Sekondari katika eneo la Dovya, kata ya Chamazi na ujenzi wa kituo cha afya Kulasini.
Miradi Manispaa ya Kigamboni iliyofuatiliwa ni ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Lingato (Kisarawe II) na ujenzi wa Nyumba ya Walimu katika Shule ya Sekondari Tundwi Songani.
"Kwa ujumla utekelezaji wa miradi hiyo umefanyika vizuri, dosari chache zilizobainika kwa baadhi ya miradi zilitolewa ushauri wa kuzirekebisha, miradi iliyobainka kuwa na dosari na ushauri uliotolewa" amesema Bw. Hazinamwisho.
Katika uelimishaji umma, TAKUKURU Temeke imefanya kazi za kuimarisha klabu za wapinga rushwa kwenye shule za Sekondari, Msingi na Vyuo, kufanya mikutano ya hadhara, semina kwenye idara mbalimbali, vipindi vya Redio na kushiriki maonesho na midahalo.
Amesema kuwa lengo kubwa ni kuzidi kuielimisha jamii kuhusu rushwa na kuifanya iweze kujua wajibu wake na namna inavyoweza kuisaidia Serikali kuwa mstari wa mbele katika kuzuia rushwa hasa kwenye miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa kwa fedha nyingi kutoka Serikalini.
Bw. Hazinamwisho amesema kuwa katika robo ya Januari - Machi, 2024 wataendelea kujiimarisha katika uzuiaji rushwa kwa kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kukabili tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma za jamii, ufuatiliaji utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema pia wataweka nguvu katika kuhamasisha ushiriki wa kila mwananchi katika vita dhidi ya rushwa kupitia Programu mbalimbali ikiwemo programu ya TAKUKURU Rafiki.
Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa TEMEKE wanaokumbana na kadhia ya matumizi mabaya ya ofisi za umma ikiwemo udanganyifu wa kutoa leseni zisizofuata utaratibu wa sheria, kanuni na miongozo wasisite kutoa malalamiko kwenye ofisi zetu zilizopo Temeke na Kigamboni ili hatua za kisheria, chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya 2007 ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Post a Comment