WADAU SEKTA YA ASASI ZA KIRAIA WAJIPANGA KUSHIRIKI WIKI YA AZAKI MKOANI ARUSHA
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Foundation For Civil Society FCS akizungumza na waandishi habari kuhusu wiki ya AZAKI ambayo inatarajiwa kufanyika Octoba 23 hadi 27 Mkoani Arusha.
.............
Na Mwandishi wetu
TAKRIBANI washiriki 500 wakiwemo wadau wakuu wa maendeleo katika sekta ya Asasi za kiraia na sekta binafsi wanatarajia kushiriki katika wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI), Mkoani Arusha itakayofanyika Oktoba 23 hadi 27, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam mapema leo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Foundation For Civil Society (FCS) Francis Kiwanga amesema wiki hiyo ya AZAKI inaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha ushirikishwaji bora na watendaji kutoka sekta mbalimbali hapa nchini.
"Tukio hili ni muhimu kwa wadau wa maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi, Serikali na wananchi"amesema Kiwanga.
Amesema tukio hili Kwa mwaka huu limejikita katika kujadili na kuweka mikakati na kuboresha utendaji wa AZAKI nchini haswa katika maswala ya Teknolojia.
Akitaja mijadala itakayojadiliwa ni pamoja na kuziwezesha na kuzipa nguvu jamii zilizotengwa, ujumuishwaji wa teknolojia kwenye kazi za AZAKI, utetezi ushirikiano na uchechemuzi wa kidigitali, data takwimu Kwa ajili ya kuleta mabadiliko, teknolojia na maadili pamoja na ubunifu wa teknolojia na maendeleo endelevu.
Kiwanga amesema katika wiki hiyo ya AZAKI itakuwa na mada tofauti zilizojikita katika kutathimini kauli mbiu ya Teknolojia na AZAKI ambazo ni pamoja na ujumuishaji na uwekezaji wa kidigitali, matumizi ya takwimu kuleta manufaa kwa jamii, teknolojia na utetezi wa kijamii, elimu na mafunzo ya dijitali nchini Tanzania.
Nyingine ni pamoja na teknolojia katika ushirikiano na kuboresha uwazi, ujasiriamali na teknolojia Kwa maendeleo endelevu, kuimarisha usalama mtandaoni, kuwawezesha wanawake na vijana kupitia teknolojia, kuweka wazi data na uwazi kwenye Utawala pamoja na kutumia maarifa bandia yanayozingatia maadili Kwa manufaa ya jamii.
Kwa upande wake mshauri mwandamizi kutoka Shirika Norwegian Church, Aneth Torjusen amesema kikao hicho pia kinalenga kujadili athari za mikopo inayotolewa na Serikali katika maisha ya watu na maeneo yanayopendekezwa kuboresha.
Naye Mkuu wa kitengo cha sekta za umma kutoka benki ya Stanbic Doreen Dominic amesema sekta binafsi inalojukumi kubwa la kuwanyanyua wananchi katika shughuli za kiuchumi Kwa kuwawezesha katika kazi zao za ujasiriamali ikiwemo biashara.
Post a Comment