Ads

TMDA YAWAJENGEA UWEZO WATAALAMU AFYA KUONGEZA UFANISI UCHUNGUZI WA DAWA, MADHARA MATUMIZI YA CHANJO

NA NOEL RUKANUGA,  DAR ES SALAAM.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imewajengea uwezo wataalamu wa Afya katika Halmashauri tano za Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya uchunguzi dawa pamoja na madhara yanayotokana na matumizi ya chanjo.


Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo timu za uchunguzi, Mjumbe wa Timu ya Usimamizi wa Huduma Afya Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Mikaji Rashid, amesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuzisaidia timu za uchunguzi kutoka kila Halmashauri ya Jijini la Dar es kufanya kazi kwa ufanisi 

Dkt. Rashid amesema kuwa elimu hiyo inakwenda kupeleka maarifa katika vituo vyao vya kazi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao.

"Timu zote za Halmashauri zinapaswa kuweka malengo ya ufatiliaji wa watumiaji wa dawa na matumizi ya chanjo ambapo wamepata madhara pamoja na kutoa taarifa kwa Mamlaka husika" amesema Dkt. Rashid.

Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Dkt. Yona Hebron, amesema kuwa wameandaa mafunzo hayo  maalumu kwa ajili ya timu ya uchunguzi dawa pamoja na madhara yanayotokana na matumizi ya chanjo.

Dkt. Hebron amesema kuwa zimeundwa timu  kutoka kila halmashauri ndani ya  Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya uchunguzi dawa pamoja madhara yanayotokana na matumizi ya chanjo.

Amesema kuwa kila timu itakuwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi.

Dkt. Hebron amesema  kuwa lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuhakikisha wajumbe wa timu za uchunguzi wanajengewa uwezo wa kufanya uchunguzi wa madhara yanayotokana na matumizi ya dawa na chanjo.

"Sheria inatutaka pale madhara yanapotokea uchunguzi unapaswa kufanyika ndani ya siku saba ili kuwezesha Mamlaka na Serikali kwa ujumla kuchukua hatua juu ya dawa ambayo imekuwa ilileta shida katika matumizi yake" amesema Dkt. Hebron.

Amesema kuwa ni muhimu timu hizo kujengewa uwezo wa kufanya uchaguzi badala ya kusubiri watumishi wa TMDA kufanya uchunguzi katika maeneo ya kazi.

Amefafanua kuwa washiriki wa mafunzo haya wamepewa nyezo mbalimbali za kufanyia kazi, kujifunza pamoja na namna ya kufatilia madhara yanayotokana na chanjo jambo ambalo ni rafiki katika kufanikisha utendaji kazi.

"Mafunzo yanakwenda kutusaidia katika kuhamasisha kutoa taarifa ya madhara yanayotokana na dawa pamoja na chanjo, hivyo kila halmashauri ikitimiza uwajibu wake tutaweza malengo tarajiwa" amesema Dkt. Hebron.

No comments