TANESCO WAJIPANGA KUZIKABILI MVUA ZA VULI.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Agosti 25, 2023 imetembelea mradi wa Bwawa la Julius Nyerere JNHPP kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa ujenzi wa mradi na kufanya tathimini ya hali ya mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwezi Oktoba hadi Disemba 2023.
Hatua hiyo imekuja baada ya Agosti 24, 2023 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa. Dkt. Ladislaus Chang'a, kutoa taarifa ya mwenendo wa mvua za vuli, ambapo ameeleza kuwa katika msimu wa mvua za vuli, mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam.
Mikoa mengeni ni Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na pamoja na visiwa vya Unguja pamoja na Pemba.
Akizungumza baada ya kumaliza kutembelea Bwawa la Julius Nyerere JNHPP, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Maharage Chande, amesema kuwa baada ya kupata taarifa ya utabiri wa mvua za vuli kutoka TMA kuwa msimu huu kutakuwa na mvua nyingi wamekuja kwa ajili ya kufanya tathmini.
Chande amesema kuwa timu ya menejimenti ya TANESCO imetembelea mradi huo kwa ajili ya kufanya tathimini kuhusu mvua zitakazonyesha miezi inayokuja.
” Endapo utabiri huo utakwenda kama ulivyopangwa basi bwawa hilo litajaa kwa haraka zaidi, zikinyesha kama ilivyotarajiwa itakuwa heri, lakini zikiongezeka tumejiandaa kwa kuweka mipango itakayohakikisha kazi za mradi zinaendelea pasipo kupata changamoto" amesema Chande.
Amesema kuwa wamejipanga kuwaanda mapema wataalamu watakaoendesha mradi huo "Tayari tumeongeza wafanyakazi zaidi ya 24 kwa ajili ya kujiandaa kuendesha mchakato huo utakapokamilika"
Katika taarifa ya utabiri wa mwenendo wa mvua za vuli, TMA imetoa ushauri katika sekta ya Nishati, Maji na Madini kuhusu upatikanaji wa maji unatarajiwa kuimarika, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani na Juu ya Wastani.
Imeeleza kuwa kutakuwa na kina cha maji katika mabwawa na mito kinatarajiwa kuongezeka. huku ikibainisha kuwa athari katika miundombinu ya rasilimali maji na nishati inaweza kujitokeza.
Imeeleza kuwa shughuli za uchimbaji madini hususan katika migodi midogomidogo zifanyike kwa kuzingatia tahadhari zinazotolewa kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi.
Wadau wanashauriwa kuzingatia matumizi endelevu na uhifadhi wa rasilimali maji katika shughuli za uchakataji wa madini, uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwandani na majumbani.
Hali kadhalika, mamlaka husika zinashauriwa kuweka mipango madhubuti ya uzalishaji wa nishati ya umeme kutoka vyanzo mbadala kama vile nishati ya jua, upepo na gesi endapo kutatokea uharibifu wa miundombinu kutokana na athari za mvua za Juu ya Wastani.
Post a Comment