Ads

VULI 2023: MVUA ZA JUU YA WASTANI HADI WASTANI ZINATARAJIWA KATIKA MAENEO MENGI YA NCHI.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa. Dkt. Ladislaus Chang'a, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2023).

NA NOEL RUKANUGA , DAR ES SALAAM.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema katika msimu wa mvua za vuli, mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam.

Mikoa mengeni ni Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na pamoja na visiwa vya Unguja pamoja na Pemba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 24/8/2023 Jijini Dar es Salaam kuhusu na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2023), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa. Dkt. Ladislaus Chang'a, amesema kuwa pia maeneo ya mikoa ya Mara, kaskazini mwa mkoa wa Simiyu, Arusha, Manyara na Kilimanjaro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Dkt. Chang'a amefafanua kuwa kutokana na uwepo wa El-Niño, vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kwa mwezi Septemba, 2023 katika baadhi ya maeneo nchini, huku akieleza kuwa mvua za Vuli, 2023 zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi Oktoba, 2023 katika maeneo mengi. 

“Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023 katika maeneo ya magharibi mwa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine mwezi Oktoba, 2023" amesema Dkt. Chang'a.

Amesema kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Disemba, msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea mwezi Januari, 2024 pamoja na ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Disemba, 2023.

Dkt. Chang’a amesema kuwa wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ikizingatiwa kuwa mwelekeo wa mvua uliotolewa ni kipindi cha msimu wa miezi mitatu.

"Viashairia vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadaliko ya muda mfupi utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi" amesema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a amesema kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika. 

"Wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao" amesema Dkt. Chang’a.

Msimu wa Mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma

No comments