Ads

PROGRAMU ZA CHUO KIKUU UDOM ZINAVYOWASAIDIA WANAFUNZI KUFIKIA MALENGO YAO.


Makamu Mkuu wa UDOM Profesa Lughano Kusiluka.

Na Francisco Peter, Dar es Salaam.

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kinawakaribisha wadau mbalimbali kujiunga masomo katika programu zaidi ya 80 zinazotolewa katika ngazi ya Shahada ya awali, Umahili katika fani ya Udaktari, Uchumi, Sheria, Sosholojia, Utawala wa Biashara, Biashara na Uhasibu, Biashara katika Rasilimali Watu pamoja na Ujasiriamali na Biashara ya Kimataifa.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2023, yanayoratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Makamu Mkuu wa UDOM Profesa Lughano Kusiluka, amesema pia wanatoa programu ya Utalii, Masoko, Mazingira, Takwimu, Ununuzi  na Ugavi, Teknolojia ya Habari na Mwasiliano (TEHAMA), Jiolojia, Kemia, Madini, Petroli, Nishati Mbadala, Elimu, Lugha, Uhusiano wa Kimataifa, Ikolojia pamoja Uandishi wa Habari na Mahusiano ya Umma na Fizikia.

Profesa Kusiluka amesema kuwa wanafunzi watakaojiunga na UDOM watapata fursa ya kufundishwa fani mbalimbali kwa umahiri ili kuwajengea hali ya kujiamini pale wanapohitimu wawe na mawazo na uwezo wa kujiajiri.

"Tunawakaribisha watanzania katika banda letu la Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) sababu hapa tunawataalamu wa kila fani ambao wanashiriki ili kutoa maelezo ya kina kwa wananchi wanaotembelea hapa,” amesema Profesa Kusiluka.

Amebainisha kuwa UDOM ni Chuo chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 32,000 na kimejengwa mahasusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii kwa kufundishwa uweledi mkubwa.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Bi. Rose Joseph amesema kuwa Chuo kina mazingira rafiki ya kujifunza na kujisomea katika kuhakikisha anafanya vizuri katika masomo yake.

Bi. Rose ameleeza kuwa pia Chuo kinatoa huduma  ya udahili wa moja kwa moja wa wanafunzi wanaotaka kujiunga kwa mwaka wa  masomo kwa mwaka 2023/24 pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu programu zinazotolewa.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika maonesho hayo ni  :  Kukuza Ujuzi nchini kupitia elimu ya juu, Sayansi na Teknolojia na Uchumi Imara na Shindani.

No comments