NHIF KUENDELEA NA UHAKIKI WA WANACHAMA WAKE MIKOA YOTE
*Ni baada ya kubaini ufanganyifu kwa baadhi ya wanachama katika mikoa sita
*Taasisi 88 kutoka sekta binafsi zawekwa chini ya uangalizi mkali
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya( NHIF) umetangaza kuendelea kufanya uhakiki wa wanachama wake baada ya kubaini uwepo wa masuala mbalimbali yakiwemo ya baadhi ya wanachama wa mfuko huo kufanya udanganyifu.
Akizungumza leo Julai 11, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bernard Konga ameelezea kwa kina hatua ambazo wameendelea kuchukua kudhibiti udanganyifu unaoendelea kufanywa na baadhi ya wanafuika wa mfuko huo.
"Mfuko umeanzishwa NHIF mwaka 2001 na umeendelea kusimamia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wanufaika wanaostahili kulingana na miongozo, taratibu na mkataba wa huduma baina ya Mfuko na Watoa Huduma.
"Kwa sasa Mfuko unahudumia takribani wanufaika 4.9 milioni ambao wanapata huduma katika vituo zaidi ya 9,000 nchini kote kuanzia ngazi ya zahanati hadi Hospitali za Taifa. Katika kipindi hicho, Mfuko umeendelea kuboresha huduma kwa kujumuisha katika kitita chake cha Mafao dawa...
" Vipimo na matibabu kulingana na maboresho yanayoendelea katika Sekta ya Afya chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita ikiongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.Mathalani kama nchi tunajivunia kuwa na huduma za ubingwa bobezi zitolewazo na Hospitali za Serikali, Binafsi na Mashirika ya Dini katika ngazi za Rufaa za Mikoa, Kanda na Taifa.
"Utolewaji wa huduma hizi unatokana na
uwekezaji katika rasilimali watu pamoja na miundombinu ya kutolea huduma hizo kama vile huduma za moyo, figo, usafishaji wa damu, saratani pamoja na vifaa vya uchunguzi kama CT SCAN (50), MRI (19), CathLab (3), LINAC (2), " amesema Konga
Aidha amesema pamoja na jitihada za kusimamia upatikanaji wa huduma bora kwa wanufaika wake, bado kumekuwa na changamoto mbalimbali katika utoaji wa huduma ikiwemo kutozingatiwa kwa masharti ya mkataba baina ya Mfuko na wadau wake ikiwemo watoa huduma na wanachama.
Amefafanua hadi kufikia Juni 2023, Mfuko umechukua hatua kwa wote waliobainika kufanya udanganyifu ikiwa ni pamoja na kusitisha mikataba 48 baina yake na watoa huduma, kuwaripotiwa watumishi 139 wa sekta ya afya katika namalaka zao za ajira yakiwemo nabaraza yao ya kitaaluma kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Pia hatua dhidi ya wanachama wachangiaji na wanufaika 1,197 wa Mfuko zimechukuliwa ikiwemo kusitisha matumizi ya kadi 697, kuamuriwa kulipa gharama za matibabu zilizotumika 325, kuwafungulia mashtaka 67 na kuwaripoti katika Mamlaka za uchunguzi (108).
"Katika kuimarisha usimamizi wa huduma za bima ya afya kwa wanachama wake, na pia kupata suluhisho la changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha kuwa wanachama wanapata huduma bora, kuanzia Juni 2023, Mfuko uliamua kuweka watumishi wake katika baadhi ya vituo kwa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma.
"Mfuko unawashukuru watoa huduma kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha kwa kipindi chote cha mwezi Juni 2023 tangu kuanza kwa mpango wa kuhakiki
wanachama na huduma.Kupitia ushirikiano huo upatikanaji wa huduma bora za afya umeimarika kwa wanufaika hivyo mpango huo ni endelevu, " amesema Konga.
Akieleza zaidi amesema tathimini ya ujumla tangu kuanza kwa mpango huo, imebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali hivyo Mfuko unaona kuna umuhimu wa kuwakumbusha wanachama wake na watoa huduma kuhusu haki na wajibu wao kama wadau muhimu kwa manufaa ya wote.
"Kwenye eneo la matumizi mabaya ya kadi baadhi ya mambo yaliyobainika
ni wanachama kutoa kadi zao kwa wasio wanachama wa Mfuko na hivyo
kupata huduma kinyume cha Sheria na utaratibu wa Mfuko. Nitoe rai kwa
wanachama kuhakikisha wanatumia kadi wao tu pasi na kumpa mtu
mwingine yoyote.
"Baadhi ya wanachama kuacha kadi zao vituoni ambapo jumla ya kadi
2,490 zimepatikana vituoni. Wanachama wanakumbushwa kuondoka
na kadi zao mara baada ya kupata huduma na si kuziacha kwani ni
kinyume cha utaratibu. Nitoe rai kwa watoa huduma kutoa taarifa ya uwepo
wa kadi kupitia Ofisi zetu za Mfuko, " amesema.
Ameongeza wanachama kudurufu na kutoa nakala za kadi na kutaka kuzitumia kupata matibabu ambayo ni kinyume cha utaratibu. Niwakumbushe kuwa kadi hizo haziruhusiwi kupata huduma
Akizungumzia upande wa utoaji wa huduma, Konga amesema imebainika baadhi ya vituo kutozingatiwa utaratibu wa uhakiki wa wanachama kabla ya huduma hivyo kuruhusu watu wasiostahili kupata huduma kwa gharama za Mfuko.
"Kutoa huduma kwa wanufaika wasiofika vituoni au kwa kuwatuma ndugu kuwachukulia dawa. Miongozo inaelekeza mgonjwa kuonwa na
Daktari na sio kupitia ndugu, jamaa na marafiki. Mfuko umetoa ridhaa kwa watoa huduma kutoa dawa za hadi miezi mitatu ili kuepusha usumbufu kwa wanachama pale ambapo anatoka mbali, " amesema.
Aidha amesema hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni kuzuia matumizi ya kadi 3,589 za wanufaika zilizokuwa na taarifa zenye shaka na kuwataka kufika kuhakiki taarifa zao kama ilivyoelekezwa awali na Mfuko.
Ameswma mfuko ulitoa tangazo mnamo Machi kwa makundi mbalimbali kufanya uhakiki wa taarifa zao ikiwemo taarifa za wategemezi wao. Zoezi hilo ni endelevu hivyo wanachama wanashauriwa kufika ofisini na kuhakiki taarifa hizo.
pia amesema kufanya uchambuzi wa matumizi ya kadi zote zilizobainika kutumika kinyume cha utaratibu na kuchukua hatua stahiki,kuzuia malipo ya huduma zote za matibabu zilizobainika kuwasilishwa kinyume na utaratibu uliowekwa na Mfuko.
Aidha kuongeza wigo wa kuweka watumishi wa Mfuko vituoni ili kuimarisha zoezi la uhakiki wa wanachama na utoaji wa huduma, uongeza wigo wa matumizi ya utambuzi wa wanachama kwa kutumia alama za vidole na sura kwa vituo vya kimkakati ikiwemo Kliniki za Kibingwa, Hospitali ngazi ya Rufaa, Kanda na Taifa.
Amesema maandalizi yameshaanza kwa kushirikiana na watoa huduma na sasa hatua hii iko kwenye majaribio na tunategemea kupeleka kwenye vituo vyote ndani ya mwaka huu.
Pia kuongeza udhibiti wa kielekitroniki katika uhakiki na uwasilishaji wa madai
kabla ya malipo, kusitisha uanachama kwa waajiri 88 ambao ni watoa huduma binafsi na wafanyakazi wao waliobainika kutumia vibaya kadi zao wa matibabu kwa manufaa binafsi.Kuendelea kutoa elimu kwa wananchama na wadau kuhusu haki na wajibu wao kwa Mfuko huu.
Pamoja na hayo amesema mkakati wa kuhakiki wanachama na utoaji wa huduma vituoni ni endelevu hivyo ametoa mwito kwa watoa huduma na wanachama wote kuendeleza kushirikiana na mfuko kwa manufaa ya wote.
"Wanachama wanakumbushwa kutimiza wajibu wao pamoja na kufahamu haki na wajibu wao kwani Mfuko huu ni wa kwao na vizazi vyao hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuulinda na kuufanya udumu.Watoa huduma wanakumbushwa kufuata miongozo yote iliyopo, taratibu na makubaliano na Mfuko katika kutoa huduma kwa wanachama ili Mfuko huu ambao ni chanzo kikubwa cha mapato kwa vituo uweze kuwa endelevu, " amesema Konga.
Post a Comment