Ads

CHONGOLO AMTAKA WAZIRI MCHENGERWA KUFIKA HARAKA HIFADHI YA RUAHA IRINGA

 


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amemuagiza Waziri wa Maliasili na utalii, Mohamed Mchengerwa kwenda katika Tarafa ya Pawaga Mkoani Iringa kushughulikia mgogoro wa Wafugaji wa Tarafa hiyo na Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.


Wafugaji wa eneo hilo wanadai kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na Askari wa Hifadhi hiyo hususani mifugo yao inapovuka mipaka na kuingia Hifadhini ambapo kwa niaba ya Wananchi Diwani wa Kata ya Mlenge, Msafiri Nzalamo amesema Kata yake inapakana na Hifadhi na hivyo huwa ni rahisi mifugo kuingia kwenye Hifadhi na hivyo kukutana na kichapo kutoka kwa Maofisa wa Hifadhi.

Akijibu malalamiko hayo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jonas Makwati amesema ufumbuzi wa tatizo hilo utapatikana na mgogoro huo utakwisha kutokana na Baraza la Mawaziri kuweka upya mipaka ya Hifadhi na maeneo ya Wananchi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amesema amemuagiza Waziri wa Maliasili na Utalii kufika katika eneo hilo na mbali ya kutatua mgogoro pia kutatua tatizo la baadhi ya Wananchi ambao walivamiwa na Tembo mashambani kwao lakini hawajalipwa fidia mpaka sasa.

No comments