Ads

BENKI YA NBC YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 6 KWA SERIKALI


Mwenyekiti wa Bodi, Benki ya NBC Elirehema Doriye (wa pili kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi Bilioni 6 kwa Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu (wa tatu kushoto), ikiwa ni gawio kwa Serikali. Hafla hiyo imefanyika leo Mei 17, 2023 Jijini Dar es Salaam.

Na Francisco Peter, Dar es Salaam.
Benki ya NBC imetoa gawio la shilingi Bilioni 6 kwa Serikali, ikiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2022.

Akiongea wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya hundi iliyofanyika leo Mei 17, Jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu ameipongeza Benki ya NBC ambayo Serikali ni mmoja ya wanahisa wa Benki ya hiyo, ikimiliki aslimia 30 ya hisa zake, amesema mafanikio hayo ni matokeo chanya ya utendaji mzuri uliowezesha kupatikana kwa faida nzuri.


“Serikali inaridhishwa na utendaji wa Benki ya NBC. Ikiwa kama mwanahisa , Serikali inafurahi kuona uwekezaji wake unakuwa wenye tija. Kiasi cha shilingi bilioni 6 tulizopokea leo, kitasaidia katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo,” amesema Mchechu.

Aidha amebainisha kuwa Ofisi ya Msajili itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Benki hiyo ili kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri zaidi na kutoa gawio kwa Serikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi, Benki ya NBC Elirehema Doriye amesema, mafanikio ambayo Benki imepata yamechangiwa na uaminifu ambao wateja wameijenga kwa Benki hiyo


“Tunayofuraha kuendelea vyema katika kuyafikia malengo yetu ikiwa ni pamoja na kujitanua na kuwekeza zaidi katika teknalojia huku tukitoa uzoefu mpya wa huduma za kibenki kwa wateja wetu.

“Faida yetu kabla ya kodi imekua kwa 36% kufikia shilingi bilioni 81.9 kutoka shilingi bilioni 60 mwezi Disemba 2021. Faida hii imetuwezesha kutoa gawio la shilingi bilioni 20 kwa wanahisa wetu ikiwamo Serikali ambayo leo tunakabidhi hundi ya shilingi bilioni 6,” amesema Doriye

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBC Theobald Sabi ameishukuru Serikali kwa kutengeneza mazingira rafiki ya Biashara ambayo yameiwezesha Benki yake kukua siku baada ya siku.

“Utendaji na faida tuliyopata ni uthibitisho wa mazingira mazuri ya Biashara ambayo Serikali Imeyatengeneza ambayo yametuwezesha kuwafikia wateja wengi zaidi na kutengeneza faida zaidi. Tutaendelea kufanya uwekezaji kwenye upanuzi wa mtandao wetu wa Kibenki na kuwekeza zaidi katika Teknalojia, ili kukidhi mahitaji ya wateja wetu” ameeleza Sabi.

No comments