TAMCODE YAPINGA ADHABU YA KIFO …YASEMA BORA HUKUMU YA KIFUNGO CHA MAISHA
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMCODE, Rose Ngunangwa Mwalongo
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) limetoa wito kwa Majaji kutoa hukumu ya kifungo cha maisha kwa washtakiwa wa mauaji badala ya kifo ili kuokoa watu wasiokuwa na hatia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkoani Kilimanjaro , Mkurugenzi Mtendaji wa TAMCODE, Rose Ngunangwa Mwalongo Leo Oktoba 10 ikiwa ni Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo Duniani amesema TAMCODE inaungana na dunia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Adhabu ya Kifo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2022 ni ‘Hukumu ya Kifo, Njia Iliyogubikwa na Utesaji.’
Mwalongo anaeleza kuwa Kauli mbiu hii inakuja wakati ambapo dunia imeshuhudia baadhi ya shuhuda juu ya waliohukumiwa kifo kuwa walikubali makosa kutokana na kushurutishwa kwa njia za utesaji.
“Iwe ni Kweli au la mchakato wa kuhojiwa unaweza kuwa na matatizo na ni vigumu sana kuthibitisha kama mtuhumiwa alitoa ushahidi kwa kushurutishwa au la. Itoshe tu kusema kuwa yapo mambo mengi ambayo yamejificha katika kila ushahidi uliotolewa”,amesema.
“TAMCODE inatambua uwepo wa Kifungu cha 197 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kinaweka bayana kuwa ‘Mtu anayepatikana na kosa la mauaji atahukumiwa kifo,’ lakini pia inatambua kwamba kumekuwepo na majaji ambao wametoa hukumu mbadala badala ya kifo, ambapo wale ambao wangehukumiwa kunyongwa, walihukumiwa kifungo cha maisha”,ameeleza.
Hata hivyo amesema shirika hilo linatambua jitihada zote za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye hajasaini hukumu ya kifo na nia njema ya kubatilisha adhabu za wale waliohukumiwa kifo, hali ambayo imeifanya Tanzania kuwa katika rekodi ya kutokunyonga tangu mwaka 1994. Hakika hili linastahili kupongezwa.
“Wakati tunapongeza nchi yetu kutokunyonga kwa muda mrefu, TAMCODE inapenda kuunga mkono wito uliotolewa na mmoja wa Majaji wastaafu wazoefu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania Madam Engera Kileo juu ya haja ya kuondoa hukumu ya kifo katika sheria kutokana na aliyenyongwa kutokuwa na nafasi ya kubatilishiwa hukumu kwani “mahakama zinaweza kufanya makosa na upo uwezekano wa kufanya makosa ya kibinadamu ambayo yanaweza kusababisha watu wasiokuwa na hatia kunyongwa”,amesema Mwalongo.
Post a Comment