Ads

TRA YAJIPANGA KUKUSANYA TRILIONI 23.65 MWAKA WA FEDHA 2022/ 2023

 

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 12.8.2022 jijini Dar es Salaam kuhusu mkakati wa makusanyo ya kodi mwaka 2022/2023.

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kukusanya Shilingi Trilioni 23.65, ikiwa ni sehemu ya bajeti kuu ya Serikali ya Shilingi Trilioni 41.48, huku mwaka wa fedha 2021/2022, walifanikiwa  walikusanya kiasi cha shilingi Trilioni 22.99.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 12.8.2022 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo, amesema kuwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 wanatarajia kukusanya Shilingi Trilioni 23.65, ikiwa ni sehemu ya bajeti kuu ya Serikali ya Shilingi Trilioni 41.48.

Bw. Kayombo amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na  kuendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa wafanyakazi na wafanyabiashara kuhusu sheria za kodi, tozo na ada zilizofanyiwa marekebisho ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa sawa na kurahisisha ukusanyaji na ulipaji kodi kwa hiari.

Amesema kuwa kwa sasa watanzania wanatakiwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kufanikisha utekelezaji wa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2022/2023.

“Tumeanza kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi, tozo na ada zinazosimamiwa na TRA pamoja na taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali jambo ambalo linaleta tija katika kukusanya kodi.” amesema Bw. Kayombo.

Amesema kuwa marekebisho na mabadiliko ya sheria za kodi yamefanyika kwa lengo la kuongeza kasi ya kufufua uchumi na kuimarisha sekta za uzalishaji kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi.

Bw. Kayombo ameeleza kuwa miongoni mwa mabadiliko ni pamoja na sheria ya usimamizi wa kodi ambayo inamtaka kila mwananchi mwenye Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

Amefafanua kuwa mabadiliko ya sheria ya usimamizi wa kodi, Sheria ya sasa inamtaka kila mwananchi mwenye namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kusajiliwa na kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) ili kumwezesha katika kufanya shughuli za kiuchumi.

“Mwaka wa fedha 2021/2022, TRA ilifanikiwa kutatua changamoto za walipakodi, kuweka mazingira mazuri ya kulipa kodi, kuongeza kasi ya kusajili walipakodi wapya, kuwekeza kwenye TEHAMA na kutoa elimu na kuhamasisha” amesema Bw. Kayombo.

Katika kuhakikisha TRA inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi wameendelea kutoa elimu katika jamii kwa nyakati tofauti ikiwemo kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa ili waweze kufikia malengo tarajiwa.

No comments