ZIARA YA MHE. WAZIRI MKUU MKOANI SINGIDA WILAYA YA IRAMBA
Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Iramba, baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa kituo cha Afya cha Mtoa, kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
…………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kufikisha huduma mbalimbali za jamii zikiwemo za afya kwa wananchi wote hadi waishio maeneo ya vijijini ili wazipate kwa wakati.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Julai 16, 2022) wakati akizungumza na wananchi katika kata ya Mtoa wilayani Iramba baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha afya cha Mtoa akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Singida.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutawawezesha wananchi hao kupata huduma za afya zikiwemo za maabara, mama na mtoto na upasuaji karibu na makazi yao. “Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza huduma za afya ziwafikie wananchi wote hadi waishio vijijini.”
Waziri Mkuu amesema kwa wilaya ya Iramba, Serikali imeidhinisha shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya sita kwa lengo la kusogeza huduma hizo karibu na makazi ya wananchi.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameupongeza uongozi wa wilaya ya Iramba kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo cha afya cha Mtoa, ambapo ameiagiza Wizara ya Fedha ya Mipango kupeleka kiasi cha shilingi milioni 262, 635,689 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema wataendelea kusimamia ukamilishaji wa kituo hicho cha afya ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma hizo karibu na maeneo yao ya makazi.
Amesema Serikali imeridhia shilingi bilioni 3.1 zitumike katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya wilayani Iramba, kati yake shilingi bilioni 2.8 ni kwa ajili ya ujenzi wa vituo sita vya afya vya Kisiriri, Mtoa, Urugu, Mwendugemba, Shelui na Tyegele na shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati sita katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
“Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya ambapo imetoa shilingi milioni 550 kwa ajili ya utekelezezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la kutolea huduma za dharura pamoja na jengo la wagonjwa mahututi katika hospitali ya wilaya ya Kiomboi. Kazi yetu ni kuhakikisha huduma zinasogea karibu makazi ya wananchi.”
Naibu Waziri huyo amesema mbali na fedha hizo, pia Serikali imetoa shilingi bilioni 7.4 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za mijini na vijiji kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ili kuziwezesha barabara za wilaya hiyo kupitika kwa wakati wote.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
“Mheshimiwa Rais Samia amefanya kazi kubwa inayobadilisha maisha ya wakazi wa maeneo haya kutokana na miradi ya elimu, maji, barabara na ujenzi wa vituo vya afya. Pia tunaiomba Serikali itusaidie ujenzi wa daraja katika mto Kinkungu ili kuwezesha mawasiliano wakati wote.”
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora amesema kabla ya mradi huo, kata ya Mtoa haikuwa na kituo cha afya, hivyo huduma za afya kwa ngazi ya kituo cha afya zilikuwa zikipatikana kata ya Shelui, ambako ni umbali wa km. 15.
Alisema kwa sasa ujenzi wa kituo hicho unaohusisha majengo sita, ambayo ni jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kufulia, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mtumishi umefikia asilimia 75.
“Makisio ya ujenzi wa majengo hayo, kwa eneo hili, ni shilingi milioni 662.6 na tulipokea shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu wa kituo cha afya, hivyo tumeiomba Serikali ituongezee shilingi milioni 262.6 ili tukamilishe ujenzi na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.”
Post a Comment