Ads

NAPE AIAGIZA TCRA KUJENGA BANDA LA KUDUMU SABASABA DSM

 Waziri  wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujenga jengo la kudumu ndani ya viwanja vya maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (DITF) ili wananchi waweze kupata huduma iliyo bora.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali, Nnauye alisema ameshaongea na Mamlaka ya Biashara Tanzania (Tantrade) kuwa TCRA ipewe ofisi ya kudumu ndani ya uwanja kwa kuwa wanamajukumu makubwa kwa jamii.

Nnauye alisema uwepo wa banda la kudumu la TCRA ndani ya maonyesho hayo litarahisha wananchi kupata huduma kwa wakati, kupunguza gharama ambazo zinatumiwa na mamlaka hiyo kila mwaka wakati wa maonyesho.

"TCRA ni wadau muhimu kwa watanzania kama mtakuwa na jengo lakudumu mtaweza kuwasaidia watanzania walio wengi kuweza kupata huduma sahihi"alisema Nnauye.Alisema Tanzania ni sehemu sahihi ya uwekezaji hivyo mawasiliano yakipatikana katika ubora itaifanya Tanzania kuwa bora zaidi.

Aidha alisema licha ya kampuni za nje kuwekeze Tanzania, TCRA isisite kutoa huduma bora kwa watanzania.

"Pamoja na huduma zote mnazotoa mtanzania anatakiwa apewe kipaumbele katika suala zima la utoaji huduma hivyo hakikisheni mnawahudumia wananchi kwa busara na upendo", alisema

Hata hivyo Nape alivitaka vyombo vyote vya habari nchini kutangaza vitu vizuri vilivyopo Tanzania ili kumuunga mkono Rais Samia Suruhu Hassan.

Vilevile aliwataka vyombo vya habari kulitangaza soko la ndani ili watanzania wavutiwe kuwekeza nchini .


Wakati huo huo, alipotembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) amezitaka taasisi za Serikali kutumia teknolojia ya TEHAMA ya kuendesha mikutano kwa njia ya mtandao (video conference).

Alisema TEHAMA hiyo itasaidia kupunguza gharama kwa serikali na itawawezesha kuwasiliana kwa urahisi zaidi kwa watumishi wao.

"Serikali ipo tayari kuwawezesha kutekeleza mpango huo wa TEHAMA, endelee kufanya kazi nzuri ya kuwahudumia watanzania," alisema


Naye Mkurigenzi wa TTCL Mhandisi Peter Ulanga alisema wao ndio wa kwanza kutekeleza agizo la Serikali la kutumia njia ya mtandao yaani video comfrence katika mikutano.

"Tuna wateja zaidi ya 10 mkoani Dodoma ambao tumeshawaunganishia huduma hiyo "alisema Mhandisi Ulanga

No comments