Ads

Jimbo la Zamfara nchini Nigeria lawaambia wakazi kuchukua silaha dhidi ya magenge ya utekaji nyara

 Mamlaka za Nigeria katika jimbo la kaskazini-magharibi la Zamfara zinatoa wito kwa wenyeji kujizatiti dhidi ya magenge ya wahalifu, katika jaribio la kukabiliana na ongezeko la idadi ya utekaji nyara na mashambulizi ya kikatili.




Wakazi wa huko lazima wajiandikishe kabla ya kupata silaha, na mamlaka ya serikali inasema hatua zinachukuliwa ili kuwaongoza watu kupitia mchakato huu.

Kuwauliza raia kujizatiti dhidi ya vitisho vya ukatili daima kutakuwa na utata. Lakini serikali ya jimbo hilo inaamini kuwa kuwapa raia silaha kutasaidia kukabiliana na ongezeko la hali ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Katika hatua nyingine, gavana wa Zamfara pia ameagiza kufungwa kwa masoko katika wilaya tatu, kupiga marufuku matumizi ya pikipiki na uuzaji wa mafuta ya petroli.

Amri ya kuua kwa risasi imetolewa kwa yeyote atakayepatikana akitumia pikipiki katika maeneo haya.

Nigeria inajitahidi kukabiliana na wimbi kubwa la utekaji nyara unaofanywa na magenge yenye silaha kaskazini mwa nchi hiyo.

Mara nyingi magenge hayo yanalenga jamii za vijijini ambazo hazina ulinzi, shule na madereva wa magari kwenye barabara kuu.

Chanzo BBC

No comments