SIDO WAKUTANA NA WADAU KUJADILI SEKTA NDOGO YA MAFUTA YA ALIZETI.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES
SALAAM
Shirika la Kudumia Viwanda
Vidogo Tanzania (SIDO) wamekutana na wadau wa sekta ndogo ya Mafuta ya Alizeti kwa
ajili ya kujadili na kuweka mipango mikakati endelevu ya namna gani wanaweza
kuboresha zao la alizeti ili liweze kusaidia Taifa kwa kuweka malengo ya muda
mfupi na mrefu.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa SIDO Mkoa wa Dodoma Bw. Stempeho Nyari,
amesema kuwa mafuta ya alizeti yameonekana kuwa uhitaji mkubwa hapa nchini
licha ya kuwepo na juhudi zinazofanywa na sekta binafsi katika kuzalishaji.
Bw. Nyari amesema kuwa SIDO
imekuwa ikitoa huduma ya kuwasaidia viwanda vidogo katika Mikoa yote inayozalisha
zao la alizeti ikiwemo Mkoa wa Dodoma, Singida pamoja na Manyara ili
kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki.
“Tumekuwa tukitoa mafunzo kwa
watu wetu na kuwapatia Teknolojia ili waweze kuzalisha mafuta yenye ubora
yaliothibitisha na Shirika la Viwango Tanzania (TBS)” amesema Bw. Nyari.
Amefafanua kuwa mpaka sasa
kuna wakulima zaidi ya milioni moja wanaolima zao la alizeti, lakini uzalishaji
bado ni mdogo ukilinganisha na uhitaji kwa watumiaji.
Bw. Nyari ameeleza kuwa
kwenye kilimo cha alizeti kuna fursa kubwa ya kiuchumi, hivyo amewataka
watanzania kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kupiga hatua katika nyanja
mbalimbali za kimaendeleo.
“Tunaendelea kuwashawishi wazalishaji
waongeze ubora wa mafuta ya alizeti, kwani sekta ndogo ya mafuta ya alizeti ina
umuhimu kwa taifa, wananchi wanaweza kujiajiri kuanzia shambani, viwandani na
kufanikiwa kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa” amesema Bw. Nyari.
Amebainisha kulingana na
ukubwa wa soko bado kuna uhitaji wa wakulima zaidi ya milioni mbili ili waweze
kuzalisha mbegu za alizeti jambo ambalo litasaidia kuongeza mchango mkubwa
katika kuchakata mafuta ya alizeti.
Akizungumza kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Kudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO), Meneja
wa Masoko wa SIDO Bi. Lilian Massawe, amesema kuwa uhitaji wa mafuta ya alizeti
hapa nchini Tanzania ni tani 650, lakini uwezo wa kuzalisha ni tani 250 hadi
300.
Bi. Massawe amesema kuwa
asilimia 70 ya uhitaji inatokana na zao
la alizeti, hivyo SIDO inaendelea kuwahamasisha wakulima na walizalishaji ili
kuongeza wigo.
“Watanzania wanatakiwa
kuja SIDO kwa ajili ya kupata ushauri wa kuzalisha zao la alizeti pamoja
kuanzisha viwanda vidogo” amesema Bi. Massawe.
Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji
wa Mafuta ya Alizeti Tanzania (TASUPA) Bw. Ringo Iringo, amesema kuwa Tanzania
ni miongoni mwa nchi zenye viwanda vingi vya kuzalisha mafuta ya kula Afrika ikiwa
na uwezo wa kuzalisha tani 3,500 kwa siku.
Bw. Iringo ameeleza kuwa
kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa mbegu za alizeti kutoka kwa wakulima,
kwani kwa mwaka wanapata tani 1,130 na kusababisha viwanda vingi kufanya kazi
chini ya uwezo wake.
Amesema kuwa maitaji ya
upatikanaji wa mbegu za alizeti kwa mwaka tani 5, 100, lakini inayopatikana
katika masoko ni tani 450 na kufanya tani 4,500 kukosekana katika soko na
kufanya kusindwa kuzalisha mafuta ya alizeti.
”Tunatakiwa kufanya uwekezaji
kwa kuwekeza katika mashamba makubwa kwa kutumia kilimo cha kisasa cha mafuta
ya alizeti, pia tunaomba taasisi za fedha wabadilishe mifumo yao ya ukopeshaji
kwa kuweka mikopo ya uwekezaji na sio mikopo ya biashara” amesema Bw. Iringo.
Katika hatua nyengine ameipongeza serikali kwa jitaida mbalimbali wanazofanya katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira marafiki ya uwekezaji.
Post a Comment