Ads

Mzozo wa Ukraine: Putin afunguka madai yake katika mazungumzo ya simu na Uturuki

 


Alhamisi mchana, Rais Vladimir Putin alimpigia simu Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na kumueleza inachokitaka hasa Urusi kwa ajili ya mpango wa amani na Ukraine.

Ndani ya nusu saa baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao ya simu, nilimhoji mshauri na msemaji mkuu wa Erdogan, Ibrahim Kalin.

Bwana Kalin alikuwa sehemu ya kundi dogo la maafisa ambao walikuwa wamesikiliza mazungumzo hayo ya simu.

Madai manne ya kwanza, kwa mujibu wa Bwana Kalin, ni rahisi kwa kwa Ukraine kuyatekeleza.

Jambo ama dai kubwa kati ha hayo ni Ukraine kukubali kwamba inapaswa kutoegemea upande wowote na haipaswi kuomba kujiunga na Nato. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky tayari amekubali hilo.

Madai mengine ni kwamba Ukraine italazimika kupitia mchakato wa kuondoa silaha (mipakani) ili kuhakikisha kuwa si tishio kwa Urusi. Lazima kulindwa kwa lugha ya Kirusi nchini Ukraine. Na kuna kitu kinachoitwa de-Nazification.

Hilo sio la kufurahisha kwa Bwana Zelensky, ambaye yeye mwenyewe ni Myahudi na baadhi ya jamaa zao walikufa katika mauaji ya halaiki ya Holocaust, lakini upande wa Uturuki unaamini itakuwa rahisi kwa Bwana Zelensky kukubali. Labda itatosha kwa Ukraine kulaani aina zote za neo-Nazism na kuhaidi kuzuia uwepo wake.

Sehemu ya pili ya madai hayo, ndipo palipo na ugumu, na katika mazungumzo yake kwa njia ya simu, Putin alisema kuwa itahitaji mazungumzo ya ana kwa ana kati yake na Rais Zelensky kabla ya makubaliano kufikiwa. Bwana Zelensky tayari amesema kuwa yuko tayari kukutana na rais wa Urusi na kufanya mazungumzo naye moja kwa moja.

Bwana Kalin hakuwa muwazi sana kuhusu masuala yaliyopo kwenye kundi la pili, akisema tu kwamba yanahusisha hali ya Donbas, mashariki mwa Ukraine, sehemu ambazo tayari zimejitenga na Ukraine na kusisitiza ni sehemu ya Urusi, na hali ya Crimea.

Ingawa Bwana Kalin hakufafanua kwa undani zaidi, ila maelezo yake yanaleta dhana kwamba Urusi itaitaka serikali ya Ukraine kuachia eneo mashariki mwa Ukraine. Hatua hiyo itakuwa ya utata sana.

Dhana nyingine ni kwamba Urusi itaitaka Ukraine kukubali rasmi kwamba Crimea, ambayo Urusi iliichukua kinyume cha sheria mwaka 2014, kwamba ni sehemu ya Urusi. Ikiwa hili litakuwa jambo wanalolitaka Urusi, basi itakuwa kidonge kichungu kwa Ukraine kumeza.

Hata hivyo, madai ya Rais Putin sio makali kama baadhi ya watu walivyohofia na yanaonekana kama hayakustahili kusababisha vurugu zote hizo, umwagaji damu na uharibifu ambao Urusi imeifanyia Ukraine.

Kwa upande wa Ukraine, hata hivyo, kutakuwa na wasiwasi mkubwa. Na makubaliano ya amani yanaweza kuchukua muda mrefu kufikiwa, hata kama kutakuwa usitishaji wa mapigano na umwagaji wa damu.

Ukraine imeteseka sana katika wiki chache zilizopita, na kujenga upya miji yajke ambayo Urusi imeiharibu itachukua muda mrefu.

credit BBC


No comments