TUME YA MADINI YAKABIDHIWA MAGARI KUBORESHA UTENDAJI KAZI.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kununua vitendea kazi ikiwemo mashine za kupima madini pamoja na kusimamia kwa ukaribu shughuli za madini ili kuhakikisha inapata mapato yake stahiki.
Akizungumza leo jijini Dar
es Salaam wakati akikabidhi magari saba kati ya magari 40 kwa Tume ya Madini Waziri
wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa magari hayo ni moja ya mikakati ya
kuboresha mazingira ya ukusanyaji wa maduhuli kwenye shughuli za uchimbaji na
biashara ya madini nchini.
Dkt. Biteko amesema kuwa
magari hayo yatatumika kama kichocheo cha ukusanyaji wa maduhuli kwenye
shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Amewataka watendaji wa
Tume ya Madini kuhakikisha magari yanatunzwa na kuendelea kuchapa kazi kwa
ubunifu mkubwa ili kuhakikisha lengo la kukusanya shilingi bilioni 650 kwa
Mwaka wa fedha 2021/2022 linafikiwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
“Mikakati iliyowekwa ni
pamoja na kuongeza maafisa kwenye
usimamizi wa shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini” amesema Dkt.
Biteko.
Waziri Dkt. Biteko
amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kuhakikisha
wanaendesha shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni za madini na kusisitiza
kuwa Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote ayakayebainika anatorosha madini.
Mwenyekiti wa Tume ya
Madini Profesa Idris Kikula, amesema kuwa magari yatarahisisha kwa kiasi
kikubwa utendaji kazi kwa kufika maeneo yasiyofikika kirahisi.
Post a Comment