Ads

MTANI HAWEKWI KOROKORONI



Adeladius Makwega-DODOMA

Utani katika jamii ya Kitanzania ni jambo la msingi mno japokuwa kwa sasa katika baadhia ya makundi wamekuwa wakijaribu kuupiga vita .hata katika misiba yao ikionekana kuwa watani ni wasumbufu.


Nimeshuhudia katika baadhi ya misiba walinzi wakitumiwa kuwazuia watani wasifanye utani huo, huku utani kwa sehemu ndogo sana misibani watani hao wakiitwa mbele na kupatiwa pesa.Hilo baadhi ya wadau wakiita huo ni utani geresha.


Kwani mtani hufanya alafu ndipo wale wanaofanyiwa utani huo wanatoa chchote kitu hicho kama asante kwake.


Huku baadhi ya wadau wa utani wakisema kuwa kitendo cha kuyaingiza baadhi ya matendo ya utani wa makabila katika makosa ya jinai kimefificha kabisa utamaduni huu.


Kwa hakika kama nionavyo mimi utani ni jambo la msingi sana kwani kwa kutumia utani huo unaweza kusaidia mno kutokutokea mabaya na madhara yaliyomkuta mtu fulani katika jamii yasimkute mtu mwingine.Watani huwa kama wafichua siri kwa midhaa.Mfichuliwa anaweza kupata aibu kwa tendo hilo


“Si uakumbuka katika msiba ule, namna watani walivyotusema, mimi sitaki aibu hii tena ijirudie katika familia yetu.” Haya huwa ni maneno ya kawaida katika familia zilizofikwa na misiba na kutaniwa na watani.


“Mabinti wa nyumba hii wanajifanya wao wazuri, hawashiriki misiba ya wenzao, hata kukuta kuni hawakati, wakija misibani hawapiki, hati wanaogopa kunuka moshi wa kuni, leo wamefiwa wao watakata kuni zao na watapika wao wenyewe.”


Niliwasikia watani wakiongea msibani huko Ikangao Mahenge-Morogoro. Hapo mwanakwetu ilibidi kuitishwa kikao cha wazee, watani waliombwa msamaha, wakapewa pombe na kuku, wakaila, ndipo taratibu zingine za msiba zikafanyika.


Nyuma ya pazia ya tukio hilo,watani walijipanga kuwa hata kama familia iliyofiwa ingeleta mpishi wa kukodi chakula hicho kingesusiwa kuliwa na pia kuzika wasingeshiriki.


Kwa faida ya msomaji wangu natoa ushauri kuwa jamii inayofanya utani na jamii nyingine ni jamii salama kuliko katika jamii ambayo watu wapo msibani ukaa kimya kimya labda kwa kutishiwa walinzi.


Katika utafiti wangu nimeabaini hata jamii zinazotumiwa walinzi kuwatisha watani, mara baada ya misiba watani wanalalamika na punde jamii hiyo ikifiwa tena wanasusiwa chakula au kubeba jeneza na watani huwa mbali nao. Huku wakiwasimanga mbona leo hamjaleta walinzi wa kutuzuia kama wakati ule?


Jambo hilo linaikumbusha jamii kuwa utani si suala la kuingilia na mtu mwingine bali watani na watani huketi na kumalizana, siyo suala la kuwekani korokoroni.


Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257


No comments