Tanzania Yajipanga Kupambana Na Ukeketaji Unaovuka Mipaka
Na Mwandishi Maalum,
Tanzania imekubaliana na Nchi za Kenya, Uganda, Somalia na Ethiopia kupambana na vitendo vya ukeketaji vinavyovuka mipaka ambavyo vimekuwa vikisababisha vifo na athari za kiafya na kisaikojia kwa watoto wa kike.
Hayo yamebainishwa wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa kupambana na vitendo vya ukeketaji vinavyovuka mipaka uliofanyika kwa njia ya Mtandao ukishirikisha wajumbe kutoka nchi hizo.
Akizungumza kwa niaba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia Mwajuma Magwiza amesema Serikali inashirikiana na wadau kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto MTAKUWWA 2017/18- 2021/2022 unaolenga kutokomeza vitendo vya ukatili ikiwemo vitendo vya ukeketaji.
Amefafanua kuwa Mpango huo unasisitiza ushiriki wa wadau katika kuvijengea uwezo vyombo mbalimbali ikiwemo Dawati la Polisi la Jinsia na Watoto na Watalaam wengine katika kuwasaidia wahanga wa vitendo vya ukatili ikiwemo vitendo vya ukeketaji.
Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha Wazee wa Mila na mangariba kuachana na Mila zenye madhara kwa watoto zinazokwamisha Maendeleo yao hasa katika Afya na elimu.
“Tanzania tumepiga hatua hadi sasa tumefanikiwa kukutana na Mangariba na wazee wa Mila na wengi wao wameridhia kuachana na vitendo vya ukeketaji katika maeneo yao hivyo kuokoa maisha ya Watoto wa kike” alisema Mwajuma.
Aidha amewahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Nchi nyingine kutafuta namna bora zaidi ya kupambana na vitendo vya ukeketaji vinavyovuka mipaka ili kuwa na jamii isiyo na vitendo vya ukeketaji.
“Vitendo hivi vya ukeketaji vimekuwa vikifanyika na kuvuka mipaka hivyo tutashirikiana kuimarisha utendaji kazi wa Polisi, Uhamiaji, Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kutoa elimu itakayosaidia kuondokana na vitendo hivyo” Alisema Mwajuma.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki zinazokabiliana na vitendo vya ukeketaji vinavyovuka mipaka na imejipanga kupambana na vitendo hivyo ili kuhakikisha mipaka ya Tanzania na nchi nyingine inakuwa salama kwa Watoto wa kike na kuondoka na vitendo vya ukeketaji.
Post a Comment